Burunge: Jumuiya ya hifadhi inayosimama kwa mtindo wa serikali -3

09Jul 2020
Salome Kitomari
BABATI
Nipashe
Burunge: Jumuiya ya hifadhi inayosimama kwa mtindo wa serikali -3
  • *Yabuni makusanyo utalii wa ndani
  • *Ilivyotikiswa miezi mitatu ya corona

UNAPOZUNGUMZIA Jumuiya ya Hifadhi za Jamii (WMA) Burunge, hapo unarejea kitu kikubwa zaidi mithili ya serikali, kwa maana ya kubeba vigezo vyote vya kiserikali, kuanzia muundo hadi matendo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Olasiti, Daud Milengori akionyesha moja ya jengo la shule mpya ya msingi iliyojengwa kutokana na mapato ya WMA. PICHA: SALOME KITOMARI

Lakini, waswahili wana msemo 'usione vyaelea vimeundwa'. Vivyo hivyo kwa Jumuiya ya Burunge, inayoteka mvuto wa umma kuanzia walio jirani na wa mbali kitaifa, ina historia yake.

 

Makamu Mwenyekiji wa WMA, Emmanuela Willium, anasimulia kwamba, Burunge ilianza kama eneo la majaribio mwaka 2003 na kanuni za kwanza za WMA zilitoka mwaka 2002.

 

Anasema kamati ndogo za maliasili za vijiji ziliunganishwa na kuunda WMA, kwa misingi ya kiikolojia na kupata kilomita za mraba 283 zilizofanyiwa usajili rasmi kisheria kuanzia Mei 2004.

 

Willium anasema makusanyo ya mapato, yalianza rasmi mwaka wa fedha 2006/07 kutoka maeneo ya uwekezaji. Hata hivyo, kutokana na dosari kadhaa, WMA ilianza kwa kusimamiwa na Halmashauri ya Babati, mahali iliko kuanzia mwaka 2012.

 

“Mwanzoni WMA ilipata asilimia 75 na 25 ilikwenda TAWA (Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania) na halmashauri. Mwaka 2006/07, zilipatikana Sh. milioni 37.4, nusu ilibaki na nyingine kwenda kwa vijiji wanachama," anafafanua.

 

Katibu wa Burunge, Benson Maise, anasema eneo hilo linaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori ya Mwaka 1998, ikipitia hatua kuanza kama eneo la majaribio kati ya mamlaka 16 za mwanzo zilizosajiliwa, yao ikiwa miongoni mwa nne zinazofanya vizuri.

 

“Kwa taratibu za uendeshaji, lazima kuwa na 'CBO' (asasi ndogo) ambayo inadhaminiwa na bodi ya wadhamini na kupata usajili kuwa na wawakilishi wa vijiji wananchama kwenye WMA, ambao wanapata kibali cha matumzi kilichopatikana mwaka 2017, kinachotoa uhalali wa kunufaika na wanyamapori,” anaeleza.

 

Katibu huyo anasema walitumia mbinu ya kuunda kanda za matumizi katika vijiji 10 vilivyoko katika kata tatu. Anafafanua kwamba zipo kanda sita za matumizi kwa wakazi katika namna ya kwamba haziwanyimi kunufaika na rasilimali za wanyamapori.

 

Makamu Mwenyekiji Willium analifafanua hilo kwamba, wajumbe wa kamati maalum iliyoko (AA) wanatoka kila kijiji na kuunda Bunge linalojadili masuala mbalimbali kwa maendeleo endelevu.

 

KANDA ZIKOJE?

Kuhusu namna zilivyo, Willium ana ufafanuzi: “Kanda hizo ni za matumizi ya wageni ambako wanaruhusu kutengeneza huduma za utalii."

 

Anaendelea: "Kanda nyingine ni ushoroba (mapito ya wanyama) na kuna vitu vinakatazwa kufanyika, ili kuruhusu wanyama kupita kutoka Hifadhi ya Taifa Tarangire kwenda Ziwa Manyara."

 

Pia, katika muundo huo, anataja ukanda mwingine wa Ziwa Manyara na Burunge, ambazo kimuundo zinalenga kulinda matakwa ya vijiji vya wavuvi na kwamba ni maeneo muhimu kwa madini chumvi yanayotumiwa na wanyama kama nyumbu. Kimsingi, ndiyo eneo la kukuzia watoto kwa kuwa ni salama na kunapatikana majani laini wanayoyahitaji.

 

Mdau na mtaalamu huyo anaendelea na ufafanuzi kwamba, asilimia 98 ya Ziwa Burunge iko ndani ya WMA na pindi linapojaa maji, hudumu kwa kipindi cha miaka saba, hali iliyochukua sura mwaka huu.

 

Anasema pamoja na umuhimu huo, shughuli za uvuvi ndani ya ukanda huo nyeti kwa wanyama, hazijapigwa marufuku, ili kuendeleza kukidhi mahitaji ya binadamu, hapo ikigusa moja kwa moja utegemezi wa vijiji kama Vilima Vitatu, Ngolei, Mwada na Sangaiwe, ambako shughuli za umwagiliaji zimetawala.

 

“Tuna ukanda wa matumizi ya jumla ambao wananchi wanaruhusiwa kukata kuni, majani, nguzo, kulisha mifugo. Lakini, hufanyika kwa kufuata utaratibu wa kuomba kibali kwenye ofisi ya kijiji. Kubwa ni kuhakikisha haiathiri eneo la utalii,” anafafanua katibu huyo.

 

Anataja ukanda mwingine ni wa uwindaji kitalii, ambao kampuni za uwindaji hupewa vibali ndani ya masharti kwamba wanahakikisha wanafanya kazi zao kwa kufuata sheria husika.

 

Pia kuna ukanda mwingine anaoutaja usioruhusiwa kwa matumizi yoyote, isipokuwa shughuli za kitafiti pekee na mahususi kwa wanafunzi wanaopatikana kando ya Hifadhi ya Taifa Tarangire.

 

UWEKEZAJI NA MAPATO

Willium anaorodhesha wawekezaji sita walionao, ambao ni Lake Burunge Tinted Lodge, Maramboi Tinted Lodge, Yulea, Tarangire River Camp, Tarangire Ospuko Lodge na wamiliki wa kitalu cha uwindaji, EBN Hunting Safari.

 

“Asilimia 75 ya mapato yote yanatokana na utalii wa picha. Mengine ni uwindaji wa kitalii na faini mbalimbali kwa wanaokwenda kinyume. Pia, tuna wahisani ambao wanaisaidia WMA kupitia huduma za kijamii na nyinginezo," anafafanua.

 

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti huyo, kasi ya ongezeko la mapato imekuwa juu kutoka Sh. milioni 37 mwaka 2006/07; mwaka 2007/08 (milioni 75.2); mwaka 2008/09 (Sh. milioni 64.5); mwaka 2009/2010 (Sh. milioni 391.4); mwaka 2010/11 (Sh. milioni 473.7); mwaka 2012/13 (Sh. milioni 275.4); na mwaka 2013/14 (Sh. milioni 412.5).

 

Vilevile, mwaka 2014/15 (Sh. milioni 820.94); mwaka 2015/16 (Sh. milioni 795.3); mwaka 2016/17 (Sh. bilioni 1.3); mwaka 2017/18 (Sh. bilioni 2.8); mwaka 2018/19 (Sh. bilioni 2.2); na mwaka 2019/20 (Sh. bilioni 2.5).

 

Anasema mwaka 2018/19 yalitokea mabadiliko ya kanuni ya kutoa mapato ya asilimia 75 kwenda TAWA asilimia 25 na halmashauri asilimia 10, na asilimia 65 inabaki WMA.

 

Makamu Mwenyekiti Willium anaeleza namna fedha hizo zinavyokusanywa na TAWA, kwa utaratibu wa mgeni wa Burunge kutakiwa kukata kibali katika ofisi maalum jijini Arusha.

 

Anaeleza namna wanavyowapokea wageni hao ni kwamba: “Tuna askari wetu kwenye kila lango ambao huhakiki vibali kabla ya mtalii kuingia. Kinachoangaliwa ni tarehe ya kuingia, kutoka na malipo aliyofanya na mwisho wa mwezi taarifa zinakusanywa na kupelekwa TAWA."

 

Makamu Mwenyekiti huyo anaeleza hatua za maboresho walizonazo hivi sasa, wameomba kutoka TAWA wawe na mfumo wa kukusanya mapato yao wenyewe, ili kuwa na uthabiti katika makusanyo yao.

 

“Tumeamua kuomba mfumo ili tuwe na utalii wa ndani, kwa kuwa kuna wananchi wanataka kutembelea hifadhi, lakini lazima waende Arusha kutafuta kibali, ndiyo waje waingie hifadhini jambo ambalo ni gharama mara mbili,” anasema.

 

PIGO LA CORONA

Katibu wa Burunge Maise anasema mwaka wa 2019/20, walikadiria kukusanya Sh. bilioni 2.5, lakini kuanzia Mach 13 mwaka huu, hawajapokea mgeni yeyote kutokana na mlipuko wa virusi vya corona. Anabainisha kuwa hadi kipindi hicho, walikuwa wamekusanya Sh. bilioni 1.4.

 

“Mgawanyo wa asilimia 65 nusu inabaki WMA kwa ajili ya uendeshaji na kwa mwaka huu, Sh. milioni 674.3 ambazo hulipa mishahara, kufanya matengenezo, kesi, mishahara, kodi za serikali na gharama nyinginezo, huku kiasi kama hicho kikienda kwenye vijiji.

 

“Mwaka 2018/19 tulikusanya Sh. bilioni 2.2 na kila kijiji kilipata Sh. milioni 100.9, lakini kutokana na janga la corona mgawo utakuwa Sh. milioni 67.5 kwa kila kijiji mwanachama,” anasema.

 

“WMA tunakusanya na kuingiza katika misingi ya uendeshaji, hadi sasa kila kijiji kimeshapata Sh. milioni 446.7 kutoka mwaka 2006 hadi 2019, na zote zimefanya shughuli za maendelea na vijiji vyetu vina ofisi nzuri tofauti na vijiji vinavyotegemea michango ya wananchi."

 

ITAENDELEA KESHO

 

Habari Kubwa