Burunge:Jumuiya ya hifadhi inayosimama kwa mtindo wa serikali-2

08Jul 2020
Salome Kitomari
BABATI
Nipashe
Burunge:Jumuiya ya hifadhi inayosimama kwa mtindo wa serikali-2

SEHEMU ya kwanza ya ripoti hii jana, ilikuwa na simulizi ya kina namna Jumuiya ya Hifadhi za Jamii Burunge ilivyozaliwa, kujiendesha na mafanikio ya juu hadi kufikia ngazi ya kijiji kuwa na mipango, bajeti na akiba, inayofanana na halmashauri zilizopo. Ufuatao ni mwendelezo wa simulizi hiyo:

Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge, Benson Maise, akionyesha moja ya matrekta lililonunuliwa na jumuiya hiyo, kwa ajili ya kulima mashamba ya wananchi na huduma nyingine katika vijiji 10 vinavyomiliki eneo la uhifadhi. PICHA: SALOME KITOMARI

Mwenyekiti wa Kijiji cha Sangaiwe, Marian Mwanso, anasema wamepata mafanikio makubwa kwa kuwa na miradi ya maendeleo kama nyumba za walimu, ofisi ya kijiji, choo cha ofisi ya kijiji, wamechangia Sh. milioni 20 katika ujenzi wa Shule ya Sekondari Mbugwe na ujenzi wa bwawa ambao wamechangia Sh. milioni 94.

 

“Uhifadhi umeimarika maana jamii inatambua WMA na tunashirikiana kiasi kwamba hakuna shughuli za kibinadamu kwenye eneo la hifadhi.

 

"Tuna Hoteli za Tarangire, Simba Lodge na Sangaiwe Tent Lodge. Tumeweka vijana wanakusanya mapato na mwisho wa mwezi makusanyo yanaingia kwenye akaunti ya kijiji na hadi sasa tuna Sh. milioni 500 benki,” anasema.

 Anabainisha kuwa kati ya fedha hizo, za WMA ni Sh. milioni 103 na Sh. milioni 400 zimetokana na mapato ya hoteli mbili zinazomilikiwa na kijiji, moja ina miaka miwili na nyingine miaka minne.

 "Miradi iliyopo kwenye mpango wa kutumia hizo Sh. milioni 500 ni kujenga vibanda kwa ajili ya uhakiki wa wageni kabla hawajaingia hotelini, ujenzi wa zahanati (Sh. milioni 84), maji, ujenzi wa madarasa mawili na ofisi. Miradi yote tuliyopanga ina fedha za kuitekeleza, hatupangi halafu ndiyo tukatafute fedha," anasema.

 

Anasema mipango ya miradi ya kipaumbele inaibuliwa na wananchi kwenye mkutano wa kijiji. 

"Nimekuwa kiongozi kabla ya kuanzishwa kwa WMA. Kabla ya WMA, michango ilikuwa kero kubwa, wananchi walishindwa kulala nyumbani na wengine kukimbia kijiji, lakini kwa sasa wamerudi na amani imetawala kwa kuwa hakuna kero,” anasema.

 Kiongozi huyo anakitaja kikwazo kilichoko katika eneo lake ni tembo kuvamia na kuharibu mazao pamoja na simba kutaka kushambulia wanyama na kuvamia binadamu, lakini wanadhibitiwa.

 

Anasema pundamilia pia wamekuwa sehemu ya vikwazo hivyo kutokana na kuharibu mazao na si wanyama walioko kwenye orodha ya fidia. 

Mjumbe wa Serikali ya Kijiji, Juliana Makseli, anasema manufaa ya WMA ni makubwa kwa kuwa watoto wao wanasoma kwa raha na walimu wana mahali pa kuishi.

 “Jamii kwa sasa haihangaiki na michango. Inapotokea, kijiji kinajua kifanyeje kupeleka na si wananchi kuchangishwa fedha,” anasema. 

KUSOMESHA WASIOJIWEZAMakseli pia anabainisha kuwa kijiji huangalia watoto yatima na wanaotoka katika familia zisizojiweza kiuchumi na kuwasomesha.

 "Tumeweka utaratibu wa kusaidia wanafunzi waliofaulu kwenda vyuo vikuu. Kila mwaka tunatenga Sh. milioni tano wanagawana kulingana na idadi yao, hii ni namna ya kuwatia moyo watoto wetu kusoma kwa bidii hadi vyuo vikuu," anasema.

 Anabainisha kuwa wapo vijana wanaosomeshwa na kijiji hicho katika vyuo vya ufundi na pia kumekuwa na utaratibu wa kusaidia kaya maskini zikiwamo za wajane.

 Mwenyekiti wa Kijiji cha Olasiti, Daudi Milengori, anasema WMA imesaidia maendeleo ya kijiji chake, akitolea mfano Shule ya Msingi Eluway ambayo kumejengwa madarasa matano, matundu 24 ya vyoo na nyumba ya walimu wawili.

 Anasema kuwa katika Shule ya Msingi Urudukai, wamejenga nyumba mbili za walimu, madarasa mawili na ofisi ya walimu, matundi 24 ya choo, madawati 40 bila mchango wa wananchi, huku wakijenga darasa moja kwa ajili ya shule ya sekondari iliyoko karibu na kijiji hicho.

 

“Fedha zinapokuja, tunaongozwa na bajeti iliyoandaliwa na halmashauri ya kijiji, inapelekwa kwenye mkutano wa kijiji unaoangalia vipaumbele. Kijiji chetu kipaumbele ni elimu na ndiyo maana tunajenga miundombinu ya elimu," anasema.

MZEE WA MICHANGO

"Ninajisikia vizuri sana, nimekuwa mwenyekiti wa kijiji kwa muda mrefu, kipindi cha michango niliwapelekesha sana kuhakikisha fedha zinapatikana mpaka nikaitwa 'mzee wa michango' na uchaguzi ulipokuja hawakunichagua tena.

 “Baada ya miaka mitano wananchi walinichagua baada ya kujua kumbe sikuwa mzee wa michango bali hatukuwa na fedha na ilikuwa lazima kurudi kwenye mifuko ya wananchi ili tufanye miradi ya maendeleo.

 

“Baada ya kuongozwa na mwingine, walinikumbuka na kunichagua awamu ya kwanza na pili na walipoona ninasimamia vizuri miradi ya maendeleo wamenichagua tena kwa awamu ya tatu. Kwa sasa, ninalala usingizi, sina kero kwa wananchi," alisifu. 

Betuel Thomas, mjumbe Kamati Maalum ya Mazingira (AA) katika Kijiji cha Vilimavitatu, anasema WMA imewaletea maendeleo na wamejenga sekondari ya kidato cha tano na sita, zahanati na shule ya msingi na zote ni za kisasa. 

“Wawekezaji wameajiri zaidi ya vijana 300 na ni wenye familia, huwezi kutembea hatua tano hujakutana na mtu aliyenufaika na WMA, tunalinda maliasili yetu bila woga,” anasema. 

Makamu Mwenyekiti wa WMA, Emmanuela Willium, anasema jumuiya hufuatilia kwa karibu utunzaji wa mazingira na vijiji vinavyoshindwa kufikia malengo, huadhibiwa kwa fedha kuzuiwa hadi watakaporekebisha kasoro. KAULI YA SERIKALI

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Babati, Hamisi Malinga, aliiambia Nipashe Mei 23 mwaka huu kuwa, halmashauri inashirikiana na vijiji kulinda shoroba ya Tarangire na Manyara kwa kuwa ni muhimu kwa uhifadhi.

 “Eneo la Manyara kuna udongo wenye madini muhimu kwa ajili ya nyumbu, lazima tushirikiane na WMA kutunza eneo hili,” alisema. 

Alisema kuwa mwaka 2004 hadi 2006, WMA iliundwa na vijiji vitano na baadaye vilifikia 10 kwa kila kimoja kutoa eneo ili kuunda hifadhi. 

Alisema vijiji hivyo vimejitegemea kwa kutekeleza miradi ya maendeleo kulingana na vipaumbele vyao na kumetoa unafuu mkubwa kwa halmashauri.

 Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, upatikanaji wa fedha umetoa ahueni kwa halmashauri kwa kuwa zaidi ya Sh. milioni 100 hupelekwa kwenye kila kijiji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutoka WMA badala ya kutolewa na serikali.

 “Imesaidia sana maana sasa wanafanya miradi wenyewe na serikali inapeleka nguvu kwingine. Kama kusingekuwa na WMA, halmashauri ilitakiwa kupeleka fedha na tungepeleka kidogo kutokana na uhaba wa rasilimali.

 “WMA ni eneo muhimu sana, linapaswa kulindwa. Kuna hoteli 17 za kitalii zinazoingiza fedha nyingi, ni ya pili kimapato baada ya Serengeti inayokusanya Sh. bilioni 2.7. WMA nyingi kwa sasa zimekufa, lakini hii imeendelea kuwapo,” alisema.

 Alisema uhifadhi umesaidia na faida zake zimeonekana kwenye ikolojia na kiuchumi ambazo zimeongeza uwezo wa halmashauri kuhudumia na kuna fedha halmashauri inapata zinaingia mfuko mkuu kwa ajili ya kutekeleza shughuli za halmashauri. Malinga alifariki dunia Juni 4 mwaka huu.

Habari Kubwa