Bwana harusi saa 72 kabla ya ndoa

08Jan 2017
Mwinyi Sadallah
Nipashe Jumapili
Bwana harusi saa 72 kabla ya ndoa

BWANA Harusi Abubakar Tursiya Haji (36), ameuawa siku tatu kabla ya kufunga ndoa kwa kupigwa mapanga na bakora, baada ya kuvamiwa na watu wanaodaiwa polisi jamii (sungusungu) huko Chuini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akizungumza na Nipashe jana, majeruhi aliyenusurika katika shambulio hilo, Juma Said Dadi (23) alisema tukio hilo lilitokea Januari 3, mwaka huu. Alisema alikwenda nyumbani kwa Haji kumsaidia matayarisho ya harusi yake iliyokuwa imepangwa kufanyika juzi.

“Niliondoka nyumbani Mwanakwerekwe na kufika saa tatu usiku nyumbani kwa marehemu (Haji) kumsaidia kupanga nyumba na shughuli zingine za ujenzi kabla ya kufanyika ndoa yake, niliamua kulala tufanye kazi mapema siku ya pili yake,”alisema Dadi ambaye amejeruhiwa vibaya kwa mapanga mgongoni na miguuni hivyo kushindwa kuinuka na kukaa mwenyewe.

Alisema alimkuta rafiki wa marehemu ambaye walikuwa wakiishi pamoja, Issa Talib Mussa, na kuanza kubadilishana mawazo wakati wakimsubiri mwenyeji wake ambaye alikuwa mjini katika harakati zake za kimaisha.

Dadi alisema ilipofika saa 3:30, waliamua kupasha wali uliokuwa umehifadhiwa na wakiwa katika mchakato huo, ghafla waliona watu wanakuja wakiwa kundi kubwa huku wakiwa na mapanga na marungu.

“Mwenzangu Issa aliniambia tukimbie, lakini mie sikuwa mwenyeji sana na njia za kule. Mwenzangu alitokea katika mlango wa dharura mie nikajificha ndani sehemu ya nyumba,” alisema.

Dadi alisema watu hao waliingia ndani na kuanza kupekua nyumba hiyo na kumwona akiwa amejificha na kumtoa kisha kuanza kumpiga kwa kutumia silaha za jadi na baadaye kuchoma nyumba moto. Baada ya kumpa kipigo hicho, alisema walimfunga na kamba miguuni na mikononi kisha kumtupia kwenye gari walilokuwa nalo na kuondoka naye.

Alisema walipofika barabarani walimwona Haji akiteremka katika gari la abiria na kumvamia na hatimaye kuanza kumshambulia kwa silaha kisha kumfunga kwa kamba mikononi na miguuni na kumpakia katika gari hilo.

“Tulipofikishwa katika kituo cha Polisi Bububu, hali zetu zilikuwa mbaya. Mahabusu tuliowakuta niliwasikia wakisema askari wapelekeni hospitalini hawa watu hali zao mbaya msiwaweke mahabusu,” alisema Dadi akinukuu kauli za mahabusu wenzao.

Hata hivyo, alisema askari waliendelea kuwaweka mahabusu na ilipofika alfajiri alikata roho. Alisema wakati wote baada ya kufikishwa kituoni hapo, Haji alikuwa akilalamika kuwa mbavu zake zimevunjika na mkono umekatika.

“Wakati askari polisi wanabadilishana zamu, majira ya saa moja asubuhi, walipoingia katika mahabusu walimkuta Haji akiwa amekufa.

Walitoa maiti yake na kuipakia katika gari na pamoja nami kunipeleka Hospitali ya Mnazi Mmoja na kulazwa kwa siku tatu,” alisema.

Naye Issa Talib Mussa, ambaye aliwatoroka sungusungu hao, alisema kabla ya mkasa wa kuvamiwa, Haji alikuwa na ugomvi na jirani yake (jina linahifadhiwa) kwa madai ya kumpiga mtoto wake, baada ya kumkamata akiiba mafenesi katika shamba lake.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir, alithibitisha kutokea kwa shambulio hilo na mtu mmoja kupoteza maisha na kwamba watu wawili wamekamatwa kwa uchunguzi.

Alisema ripoti ya uchunguzi iliyofanywa na daktari bingwa wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dk. Marijani Msafiri, imesema chanzo cha kifo cha Haji ni kipigo alichokipata katika sehemu za mwili wake.

Habari Kubwa