CAG afichua wanyamapori maelfu wanavyouawa ajali za barabarani

09Apr 2020
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
CAG afichua wanyamapori maelfu wanavyouawa ajali za barabarani

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amebaini ufuatiliaji duni wa mauaji ya wanyamapori kupitia ajali za barabarani nchini.

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, picha mtandao

Katika ripoti yake kuhusu Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2018/19, CAG Kichere anasema Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) linakabiliwa na tatizo la mauaji ya wanyamapori kutokana na ajali hizo, akibainisha kuwa jumla ya wanyamapori 2,266 waliuawa katika mwaka mmoja tu ulioishia Juni 30, 2019.

Anasema pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa mauaji ya wanyamapori unaofanywa na Tanapa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwenye barabara kuu, bado kuna matatizo mbalimbali yanayosababishwa na kuwa na teknolojia duni kama vile kukosa kamera za barabarani, jambo linalosababisha kushindwa kutambua wahusika wanaosababisha ajali hizo.

"Mapitio yangu ya ripoti ya kitengo cha ulinzi wa wanyamapori, yaligundua kuwa katika Hifadhi ya Taifa Mikumi (Minapa), jumla ya wanyamapori 124 wa aina tofauti waliuawa katika kipindi cha robo tatu ya mwaka.

"Kutokana na idadi hiyo ya vifo vya wanyamapori mbalimbali, Hifadhi ya Taifa Mikumi ilitakiwa kupokea kiasi cha fedha Sh. milioni 56.64 za tozo na adhabu za kusababisha ajali. Hata hivyo, hifadhi hiyo ilipokea Sh. milioni 12.45 tu, sawa na tofauti ya Sh. milioni 44.18.

"Menejimeti ilieleza kwamba, ajali nyingi za barabarani zinatokea wakati wa usiku, hivyo kushindwa kuwaona wanaofanya makosa kutokana na kukosekana kwa kamera za ulinzi.

"Vilevile, katika hali nyingine, malipo yalikuwa yanajadiliwa kutokana na ukweli kwamba Tanapa haina sheria ndogo za kutoza faini na adhabu, ambapo tozo au faini hutolewa kulingana na Kanuni za Taifa za Uhifadhi wa Wanyamapori, ambazo hazimfungi mtu katika mahakama za sheria.

"Ninapendekeza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania na Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro zitunge sheria ndogo na kuzisimamia ipasavyo. Vilevile, zibuni na kusimamia njia mbalimbali za usalama kama vile kuweka kamera za barabarani ili kudhibiti ajali za barabarani na hivyo kulinda wanyamapori," anashauri.

Habari Kubwa