CAG agundua janga mitaani

14May 2018
Na Mwandishi Wetu
 DODOMA
Nipashe
CAG agundua janga mitaani

WAKATI ujenzi wa majengo makubwa na marefu unaendelea kushika kasi katika miji mingi nchini, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini majengo mengi ya umma nchini si salama kwa moto.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Hiyo inatokana na kubaini kuwa mengi hayakidhi viwango na vigezo vinavyohitajika kwa usalama dhidi ya majanga ya moto.

Katika ripoti yake ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usalama katika makazi ya watu kwa mwaka 2016/17 iliyowasilishwa bungeni mjini hapa mwezi uliopita, CAG Prof. Mussa Juma Assad anabainisha kuwa majengo mengi ya umma nchini si salama dhidi ya moto kutokana na utekelezaji duni wa hatua za usalama dhidi ya moto kwenye majengo hayo.

Anasema ukaguzi wake ulibaini Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji hakikuwa na mpango madhubuti wa kukagua na kufuatilia shughuli za ujenzi na kuhakikisha majengo yote ya umma yanakaguliwa kwa ubora wa juu.

"Kutokana na hali hiyo, majengo mengi yanayotumiwa na umma yako katika hatari kutokana na utekelezaji hafifu wa mahitaji ya usalama dhidi ya moto," anaeleza Prof. Assad katika ripoti hiyo.

Anasema ukaguzi wake ulibaini utekelezaji wa miradi ya maendeleo pia haukuwa rafiki kwa usalama wa makazi ya watu.

Anasema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, jumla ya vibali vya ujenzi 17,692 vilitolewa lakini ni miradi 24 tu ndiyo ilikuwa imefanyiwa tathmini ya athari za mazingira.

"Baadhi ya miradi ya maendeleo iliyokubalika kutekelezwa, imekuwa vyanzo vya mafuriko na uchafuzi wa mazingira, hali inayohatarisha usalama wa binadamu. Mfano, ujenzi wa ofisi za Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka pale Jangwani," anasema.

Prof. Assad anaongeza kuwa ukaguzi wake ulibaini Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) hazijaweza kudhibiti matumizi ya ardhi kutokana na miji mingi kutojengwa kiutaratibu kwa sababu ya ukosefu wa mpango kabambe wa mipango-miji.

"Katika mji uliopangiliwa, maeneo mengi ya wazi hayajasajiliwa na utekelezaji wake ni kinyume cha mipango iliyowekwa," anasema na kutoa mfano kwamba:

"Matumizi ardhi yalibadilishwa kutoka maeneo ya viwanda na kuwa makazi ya watu au kinyume chake."