CAG Assad bado gumzo bungeni

16Apr 2019
Sanula Athanas
Dodoma
Nipashe
CAG Assad bado gumzo bungeni

UAMUZI wa Bunge kutofanya kazi na Prof. Mussa Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), limeendelea kuwa gumzo bungeni, safari hii chombo hicho cha kutunga sheria kikitangaza kufuatilia habari iliyoandikwa na moja ya magazeti ya kila siku kuhusu suala hilo.

Prof. Mussa Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), picha mtandao

Mara tu baada ya kumalizika kwa kipindi cha 'Maswali' bungeni jana asubuhi, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema), alisimama na kuomba kutoa hoja Bunge lijadili kile alichoeleza gazeti hilo limeingilia haki za Bunge kufuatia kuchapisha habari yenye kichwa "Bunge lamtupa CAG".

Mnyika ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, alisema kilichoandikwa na gazeti hilo kinakinzana na azimio la Bunge la kutofanya kazi na Prof. Assad.

Huku akieleza kuwa hana uhakika kama wabunge wote wamelisoma gazeti hilo na kubaini ukweli wa kinacholalamikiwa na Mnyika, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, aliyekuwa anaongoza kikao cha Bunge, alimpa dakika tatu mbunge huyo kueleza msingi wa hoja yake.

Mnyika alisema toleo la juzi la gazeti hilo liliandika habari yenye kichwa "Bunge lamtupa CAG" na kueleza kuwa chombo hicho cha kutunga sheria kimemtaka Prof. Assad akajieleze kwa Rais John Magufuli.

"Ninachofahamu Bunge halijawahi kuazimia jambo kama hili, kilichoazimiwa na Bunge ni kutofanyakazi na CAG na siyo kumtaka akajieleze kwa Rais Magufuli. Habari hii imeingilia haki za Bunge," Mnyika alisema.

Baada ya Mnyika kujenga hoja yake, Naibu Spika (Dk. Tulia) alisema hana uhakika kama habari hiyo imeandikwa kwa kuingilia haki za Bunge na si wabunge wote wameisoma.

Kiongozi huyo wa Bunge alisema hoja ya Mnyika itafanyiwa utaratibu wa kawaida kwa kulipitia gazeti hilo kisha wabunge watajulishwa kama kuna kifungu cha Sheria ya Kinga na Madaraka ya Bunge kilichovunjwa.

Aprili 2, mwaka huu, Bunge liliazimia kutofanya kazi na CAG Assad baada ya Kamati yake ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumtia hatiani kutokana na kauli yake ya mwanzoni mwa mwaka jijini Newyork, Marekani kwamba anafikiri "huo ni udhaifu wa Bunge".

Prof. Assad alifika mbele ya kamati hiyo kuhojiwa na akasisitiza neno 'udhaifu' lililolalamikiwa, si tatizo kwa kuwa katika lugha yao ya kiuhasibu linamaanisha 'upungufu'.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, Prof. Assad hakuwa tayari kujutia wala kuomba radhi kwa kulitumia neno 'udhaifu' dhidi ya Bunge na alisisitiza ataendelea kulitumia.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari ofisi kwake jijini Dodoma Jumatano iliyopita, Prof. Assad alisisitiza atendelea kulitumia neno 'udhaifu'.

Katika ripoti yake ya ukaguzi wa mwaka 2017/18, Prof. Assad pia amelitumia neno hilo dhidi ya taasisi mbalimbali ambazo alibaini zina dosari katika hesabu zake.

Habari Kubwa