CAG aweka msimamo mzito

15May 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
CAG aweka msimamo mzito

MDHIBITI na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, amesema maofisa wa ofisi yake wanatakiwa kufanya kazi kwa kujiamini na kutoogopa chochote wanapotekeleza majukumu yao.

MDHIBITI na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Profesa Assad aliyasema hayo jana jijini Dodoma wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa ofisi yake na kusisitiza kuwa wanapaswa kuhakikisha wanajibu hoja kwa wakati ili kuonyesha msimamo kwenye kazi zao.

Alisema hakuna sababu ya watumishi wa ofisi hiyo kuwa na woga katika utendaji wao, hivyo wanapaswa kuwa mfano ili kufanya kazi kwa ufanisi.

Kwa mujibu wa CAG, kuna baadhi ya mifumo ambayo inahitajika katika ukaguzi ambayo alisema wakiipata watafanya kazi vizuri.

Mbali na hilo, Prof. Assad aliwapongeza viongozi waliochaguliwa kwa ajili ya kuongoza baraza hilo na kuwataka kufanya kazi na wasibweteke.

Alisema viongozi wa baraza hilo wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanasukuma gurudumu hilo kwa maslahi ya wafanyakazi.

"Nawaomba mchape kazi na msibweteke," alisema Professa Asad.

Naye mgeni rasmi katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Utumishi), Dk. Francis Michael, alisema utovu wa nidhamu na rushwa katika mabaraza havitakiwi kabisa.

Alisema kinachotakiwa ni kufanya kazi kwa bidii ili waweze kusaidia wafanyakazi kwa ujumla.

Alisema bajeti zinatakiwa zijadiliwe na Baraza kabla ya kupelekwa bungeni ili kuhakikisha wanazitendea haki.

Habari Kubwa