CAG: Kuna uhaba mkubwa watumishi serikalini

17Apr 2019
Sanula Athanas
Dodoma
Nipashe
CAG: Kuna uhaba mkubwa watumishi serikalini

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, amebaini changamoto ya uhaba wa watumishi serikalini.

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, picha mtandao

Katika ripoti yake ya ukaguzi wa mwaka wa fedha 2017/18 iliyowasilishwa bungeni na serikali Jumatano iliyopita, CAG Assad anabainisha ameangalia kwa mara nyingine tena changamoto ya uhaba wa watumishi katika taasisi mbalimbali.

Katika ripoti yake hiyo, Prof. Assad anabainisha kuwa changamoto hiyo ina athari kubwa katika utoaji wa huduma na ufanisi wa taasisi.

“Mapitio niliyofanya katika ofisi kama za wizara, wakala, sekretarieti za mikoa na balozi 62 yanaonesha kwamba watumishi waliopo ni 9,714 ukilinganisha na mahitaji ya watumishi 19,469, hali ambayo inapelekea upungufu wa watumishi 9,755, sawa na asilimia 50.1 ya mahitaji,” Prof. Assad anabainisha katika ripoti yake hiyo.

“Kuendelea kwa tatizo hili kunahatarisha utendaji kazi wa taasisi ikiwamo utoaji wa huduma hafifu kutokana na mlundikano wa kazi na kuchoka kwa watumishi waliopo.

“Ukilinganisha na taarifa yangu ya ukaguzi uliopita (2016/17), upungufu wa watumishi unaonekana kushuka kutoka watumishi 34,081 katika taasisi 52 kwa ukaguzi uliopita hadi kufikia watumishi 9,755 katika taasisi 62 katika mwaka huu wa ukaguzi, hii ina maana ya kuwa nafasi zilizowazi bado zinaendelea kujazwa.

“Nawashauri maofisa masuuli wote kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora kujaza nafasi zilizowazi au kufanya upya mapitio ya uhitaji wa watumishi ukilinganisha kwa watumishi waliopo na huduma zinazotakiwa kutolewa.

HAKUNA MAFUNZO

Katika ripoti yake hiyo, CAG Assad pia anabainisha changamoto ya kutozingatia mafunzo kwa watumishi, akieleza kuwa Kanuni namba G.1 (7) ya Kanuni za Kudumu za Watumishi wa Umma za Mwaka 2009 inasema kuwa, taasisi zote zinatakiwa kuandaa mafunzo maalum kwa watumishi waliopo kazini kwa kuzingatia mahitaji ya mafunzo yaliotambulika wakati wa utendaji kazi zao.

“Kila taasisi itatakiwa kutenga bajeti katika mwaka wa fedha kwa ajili ya mafunzo.

“Nilipopitia nyaraka katika taasisi mbalimbali, niligundua kuwa kuna taasisi tano hazikufanya tathimini ya mahitaji ya mafunzo wala kuwapo kwa mpango wa mafunzo kwa watumishi waliopo kazini," Prof. Assad anaeleza katika ripoti yake hiyo.

Anaitaja taasisi alizobaini zinakabiliwa na changamoto hiyo kuwa ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Kuzuia Dawa ya Kulevya, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi.

CAG Assad anasema kukosekana kwa tathmini ya mahitaji ya mafunzo na kutofanya mafunzo kwa watumishi kunahatarisha ufanisi wa taasisi husika kwa kuwa watumishi watashindwa kujiendeleza katika utendaji wao wa kazi
kuendana na uhitaji wa wakati huo kama vile maboresho ya taratibu mbalimbali, kutumia vifaa vipya vilivyoanzishwa na taasisi na mabadiliko ya sheria.

“Hivyo ninawashauri maofisa masuuli wote kufanya tathmini ya uhitaji wa mafunzo kwa watumishi, kuandaa mpango wa mafunzo kwa watumishi wake kulingana na udhaifu ulioonekana kwa watumishi hao wakati wa utendaji wao wa kazi, kuandaa bajeti na kutekeleza mpango wao wa mafunzo kwa ajili ya uhai wa utoaji huduma katika taasisi,” Prof. Assad anapendekeza katika ripoti yake hiyo.