CAG naye akaguliwa

17May 2019
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
CAG naye akaguliwa

RIPOTI ya ukaguzi wa hesabu za Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) kwa mwaka wa fedha 2017/18, imekabidhiwa bungeni.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya Mwaka 1977, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ndiye mkuu wa NAOT.

Akitoa taarifa bungeni jana, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema amepokea ripoti ya ukaguzi wa hesabu za ofisi hiyo kwa mwaka unaoishia Juni, 2018 na kuipa jukumu Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuipitia na kuichambua.

"Katika ukaguzi wa hesabu, CAG kwa mujibu wa Kifungu cha 46(1) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma, Sheria Namba 11 ya Mwaka 2008, hesabu za CAG zinapaswa kukaguliwa angalau mara moja kwa mwaka na PAC huwa ina jukumu la kuteua mkaguzi wa kukagua hesabu za ofisi hiyo," alisema.

Alisema Bunge ndiyo linatafuta mkaguzi wa hesabu hizo na ripoti aliyoipokea, ilifanywa na kampuni ya ukaguzi wa Hesabu ya EK Mangesho & Company.

"Katika hesabu zilizowekwa mezani wakati ule hesabu za ofisi ya CAG huwa haziwekwi mezani pale. Sasa utaratibu ni huu ninaoeleza. Nimepokea taarifa hii na nimeipitia, kuna mambo... na utaratibu ni kupeleka PAC watapitia na kuichambua na kuwasilisha kwangu, mengine yatafuata," alisema.

Spika Ndugai alisisitiza kuwa katika masuala ya ukaguzi hakuna ambaye anabaki na hakuna anayejikagua bali kila watu wanaangalia wenzao.

Aprili 13, mwaka jana, CAG Prof. Mussa Assad, aliwaambia waandishi wa habari bungeni jijini Dodoma kuwa ofisi yake nayo huwa inakaguliwa na mkaguzi wa nje.

Habari Kubwa