CAG uso kwa uso Kamati ya Bunge leo

21Jan 2019
Gwamaka Alipipi
DAR ES SALAAM
Nipashe
CAG uso kwa uso Kamati ya Bunge leo

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, leo anatarajia kuhojiwa katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge dhidi ya kauli yake anayodaiwa kuitoa akiwa ughaibuni kuwa ‘Bunge ni dhaifu’.

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimtaka CAG, Prof. Assad, kufika mbele ya kamati  hiyo leo kujieleza kuhusu kauli yake hiyo aliyoitoa akiwa Marekani.

Akiwa nchini humo, CAG Prof. Assad, alihojiwa na chombo cha habari cha Idhaa ya Amerika juu ya ripoti za ukaguzi ambazo zimekuwa zikifanywa na ofisi ya CAG, lakini hazifanyiwi kazi pamoja na kuonyesha kasoro katika matumizi ya fedha za umma.

Kwenye maelezo yake Prof. Assad anadaiwa kueleza kuwa “sasa hili jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge, kama ofisi yake inatoa ripoti inayoonyesha ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwake mimi ni udhaifu wa Bunge, Bunge linatakiwa lisimamie na lihakikishe kwamba kwenye matatizo hatua zinachukuliwa.”

Kutokana na kauli hiyo, Januari 6, mwaka huu Spika Ndugai aliagiza CAG Assad kufika mbele ya kamati hiyo ili kujieleza kwa nini anaudhalilisha mhimili huo.

Hata hivyo, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Prof. Assad alieleza kuwa majibu aliyoyatoa wakati akihojiwa hayakuwa na nia ya kulidhalilisha Bunge.

“Maneno kama udhaifu na upungufu ni lugha ya kawaida sana kwa wakaguzi katika kutoa maoni ya utendaji wa mifumo ya taasisi mbalimbali, ni wazi kwamba watu wengine wanaweza kuchukua tafsiri tofauti ya maneno kama haya,” alisema Prof. Assad.

Mbali na kueleza hivyo, Prof. Assad, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa ataitikia wito wa Spika Ndugai wa kufika katika kamati hiyo leo kuhojiwa.

Habari Kubwa