Canada yapigia debe wanawake kiuchumi

20Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Canada yapigia debe wanawake kiuchumi

SERIKALI  ya Canada imezitaka taasisi  binafsi  kuongeza  ushiriki  wa  wanawake  katika  sekta  muhimu za kiuchumi.

Akizungumza  katika maadhimisho  ya nane ya jukwaa  la  Canada na Tanzania katika uwajibikaji  wa pamoja  kwa  jamii, Balozi wa Canada nchini, Pamela Donnell, alisema ushiriki wa wanawake katika  shughuli za kiuchumi unaongeza  uzalishaji  na usawa kwa  maendeleo  endelevu.

Balozi huyo  alisema  kampuni  binafsi zitafaidika kwa kiwango kikubwa zikiongeza nafasi za ajira kwa wanawake  na  kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi kwa kuwa takwimu zinaonyesha kampuni zenye kiwango kikubwa  cha uwakilishi wa wanawake katika za uongozi, zilipata uzalishaji mkubwa  kulinganishwa  na zile zenye uwakilishi  hafifu.

“Kampuni  zenye  kiwango kikubwa  cha usawa  wa kijinsia katika nguvu kazi yao  na uongozi  wa  juu, huvuna faida nyingi,” alisema.

Alisema  serikali ya Canada  imedhamiria  kuweka mazingira mazuri ya kibiashara na kuhakikisha  kampuni  za nchi hiyo  zinazofanya kazi katika mataifa mbalimbali,  zinaheshimu  haki  za  binadamu, sheria, miongozo, kanuni  na viwango vya kitaifa vya kibiashara kwa ushirikiano  wa serikali na  jamii.

Naye  Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kituo cha Uwekezaji  Tanzania (TIC),  John Mnali, alisema kituo hicho kinaelewa  kuwa wanawake katika sekta binafsi hukutana na changamoto mbalimbali  pamoja na upungufu wa mitaji, hivyo kusababaisha uzalishaji  kidogo  na usiokidhi mahitaji  yao na  ya familia.

Alisema Canada na Tanzania ni marafiki na zimeendelea kufanya  kazi  pamoja  katika juhudi  za kuvutia wawekezaji  wa kimataifa  wenye uwezo na viwango  katika  kufanikisha safari ya  Tanzania ya viwanda  na kwamba wanawake ni wazalishaji  wakubwa wa familia na taifa.

“Tanzania  na Canada  wamekuwa  marafiki wazuri  na ninaelewa  kuwa  serikali ya Canada inaisaidia Tanzania katika kupunguza  umaskini kwa kuzingatia mahitaji ya binadamu hasa wanawake na watoto,” alisema Mnali.

“Wanawake ndio wazalishaji  wakubwa  katika  familia nyingi. Wanawake wa  Tanzania wanapaswa kupewa uwezo  na  usawa  katika kutawala  uchumi,” aliongeza.

Naye  Kiongozi wa  timu ya mpango  wa ukuaji wa kiuchumi kutoka  Canada,  Nathalie Garon,  alisema  Canada  ni mshirika  mzuri wa Afrika na hasa  Tanzania  kwa kuwa  ina malengo yanayofanana  katika kukuza uchumi  kwa kuzingatia upatikanaji wa masoko, uwajibikaji wa kibiashara na maendeleo endelevu.

Habari Kubwa