CCBRT yafagilia muongozo wa uratibu wa NGOs

26Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
CCBRT yafagilia muongozo wa uratibu wa NGOs

Hospitali ya CCBRT imeeleza kuridhishwa na huduma zinazotolewa na Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini zikilenga kuboresha upatikanaji wa Huduma bora kwa wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi katikati akiwaonesha kitu kwenye simu yake maafisa kutoka Ofisi ya Msajili wa Mashirika yasiyo ya kiserikali nchini walipotembelea Hospitali ya CCBRT.

Hayo yamebainika jijini Dar es Salaam wakati maafisa kutoka Ofisi ya Msajili wa Mashirika yasiyo ya kiserikali nchini walipotembelea Hospitali ya CCBRT  kujionea shughuli zinazofanywa na Hospitali hiyo.

Akizungumza wakati wa ugeni huo Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi, ameishukuru Serikali kwa kuweka utaratibu mzuri wa NGOs kujisajili, kuwasilisha taarifa na mazingira rafiki ya utekelezaji wa majukumu yao.

Mkurugenzi huyo ameeleza kufurahishwa na namna ofisi hiyo ya msajili  wa mashirika inavyowajali na kuwathamini kwa  kuwatembelea wadau wake na kuona namna wanavyofanya kazi na changamoto zinazowakabili.

"Siku zote tunajivunia kuwa na Serikali ya aina hii mnatutembelea hospitalini kwetu na katika maeneo mengine tunayofanya kazi kwa ajili ya kutuunga mkono na kutushauri katika kuboresha kile tunachokifanya" amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa msafara kutoka Ofisi ya Msajili wa NGOs, Faki Shaweji, ameeleza kuridhishwa kwake na huduma zinazotolewa hospitalini hapo na kuongeza kuwa CCBRT ni moja ya mashirika yanayoisaidia Serikali kutoa huduma muhimu kwa jamii.

Faki, amesema kuwa Ofisi ya Msajili wa NGOS imefarijika kuona shughuli zinavyofanyika kwa viwango vya hali ya juu na Watanzania wanapata huduma nzuri ambazo zimewasaidia wengi wao kuondokana na matatizo yaliyokuwa yanawakabili.

 "Tumekuja hapa kama Ofisi ya Msajili wa NGOs  timu imejionea jinsi CCBRT inavyotoa huduma ambazo ubora wake unathibitika" amesisitiza

Aidha ameutaka uongozi wa CCBRT kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu kanuni na miongozo inayotolewa na Serikali ili kuboresha huduma kwa walengwa.

"Pale mnapopata changamoto msisite kupata ufafanuzi kutoka ofisini kwetu na ofisi zetu zipo wazi kwa ajili yenu wadau wetu" amesema

Ameongeza kuwa Wizara imerahisisha shughuli mbalimbali za masuala ya NGOs  kwa kuanzisha mfumo wa utoaji huduma kupitia mtandaoni kama vile usajili wa NGOs pamoja na uwasilishaji wa taarifa mbalimbali kutoka katika Mashirika hayo.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya uzinduzi wa  Muongozo wa Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara ambao unaotoa muelekeo mpya wa uendeshaji wa NGOs hasa katika kuwa na uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya pesa za miradi.

Habari Kubwa