CCM: Katiba Mpya ni muhimu

23Jun 2022
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
CCM: Katiba Mpya ni muhimu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesisitiza umuhimu wa uwapo wa Katiba Mpya kwa kuzingatia mazingira ya sasa na kuangalia namna bora ya kufufua na kukwamua mchakato wake.

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka.

Pia imeshauri serikali kuangalia namna nzuri ya kumaliza kwa haraka kesi za kisiasa zinazowakabili wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Akizungumza jana na waandishi wa habari kuhusu vikao vya juu vya chama hicho ikiwamo cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alisema mchakato huo ukwamuliwe na kukamilika kwa maslahi ya taifa na maendeleo kwa ujumla.

Aidha, alisema NEC inapongeza juhudi zote za vyama vya siasa katika kutengeneza maridhiano hayo ya kisiasa ambayo yana dhamira ya kuwaunganisha Watanzania.

“CCM inashauri serikali kuharakisha mambo yote ambayo Rais Samia alitoa dira na mwelekeo na wanasiasa wamepokea na yanakwenda vizuri,” alisema.

 

KESI ZA KISIASA

Kuhusu mazungumzo kati ya CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Shaka alisema mazungumzo yanakwenda vizuri na NEC imepokea taarifa ya mazungumzo hayo na imeshiriki hatua zote ili dhamira ya Rais Samia itimie.

“Tayari vikao viwili vimeshakaa upande wa CCM na CHADEMA na mazungumzo yanakwenda vizuri kwenye hayo mazungumzo tumeshauri serikali ikaangalie kesi zile za wanachama za kisiasa ambazo zipo kwenye vyombo mbalimbali vya kisheria kwa mujibu wa Katiba ya nchi, lakini kuangalia namna nzuri ya kumaliza haraka zaidi kesi hizo,” alisema.

Alisema nia ni kuhakikisha malengo na azma ya maridhiano inatimia.

Shaka alisema NEC imempongeza Rais Samia kwa dhamira na maono yake ya kuhakikisha milango ya maridhiano inaendelea kwa hatua kubwa ili kuhakikisha kunakuwapo na maridhiano ya kisiasa nchini.

Pia alisema NEC imempongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi kwa namna anavyoleta muafaka wa kisiasa na CCM imeahidi kumpa ushirikiano ili kuleta ustawi wa amani na utulivu wa Zanzibar.

UTEUZI

Alisema Kamati Kuu ya CCM pamoja na mambo mengine ilifanya uteuzi wa wagombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe na Halmashauri ya Ngorongoro na Manispaa ya Moshi.

WASSIRA AULA

Katibu huyo alisema NEC imefanya uchaguzi wa wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM wawili kwenye nafasi mbili zilizokuwa wazi na amechaguliwa Stephen Wassira na Theresia Mtewele.

UCHAGUZI CCM

Kuanzia Julai 2, mwaka huu, fomu za kuwania nafasi ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa zitatolewa hadi Julai 10, mwaka huu.

Habari Kubwa