CCM sasa yajitosa ruzuku ya pembejeo

14May 2022
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
CCM sasa yajitosa ruzuku ya pembejeo

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeziagiza Wizara ya Fedha na Mipango na ya Kilimo kuharakisha uandaaji wa muundo wa namna ya kutoa ruzuku ya mbolea ili kuwapunguzia mzigo wa gharama wakulima katika msimu ujao wa kilimo.

Uandaaji wa utaratibu huo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa hivi karibuni jijini hapa alipokuwa akigawa vitendea kazi kwa maofisa ugani nchini.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, alitoa agizo hilo jana alipotembelea ujenzi wa kiwanda cha uzalishaji mbolea ya asili cha Itracom, kinachojengwa na mwekezaji kutoka Burundi ambacho kinagharimu zaidi ya Sh. Bilioni 480.

Alisema wizara hizo zinatakiwa hivi karibuni ziweke wazi namna zitakavyotekeleza utaratibu huo.

“Kwenye mkutano wa maofisa ugani, Rais alitoa agizo kwa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha kukaa pamoja kuweka utaratibu wa kuhakikisha inatengeneza uhakika wa upatikanaji wa mbolea kwa bei nzuri isiyo mzigo kwa mkulima,” alisema.

Alisema mbolea inayohitajika nchini ni tani 700,000 na kiwanda hicho kitazalisha tani 600,000 kwa mwaka baada ya kukamilika na kwa awamu ya kwanza uzalishaji utaanza kati ya Juni na Julai, mwaka huu, ambapo zitazalishwa tani 200,000.

“Kwa hiyo kwa mwaka ujao tutakuwa na upungufu wa tani 500,000 ambazo unahitajika mpango ili mkulima apate mbolea, kwa hiyo tumeona hili jambo lisipite hivi tuhakikishe kunakuwepo na uhakika wa mbolea na uhakika wa utekelezaji wa maagizo ya Rais ya kuondoa changamoto ya mbolea katika msimu ujao,”alisema.

Kuhusu Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Chongolo alisema lazima sasa ifanye kazi kibiashara, kiushindani kwa kusimamia wanakuwa daraja la kuangalia bei ya mbolea na upatikanaji rahisi wa bidhaa ya mbolea bila kufanya hivyo haitakuwapo haja ya uwapo wao.

Aliagiza  ruzuku hiyo ilenge kukuza tija ya uzalishaji wa mbolea ya ndani ya nchi ili kulinda wawekezaji na kuhamasisha wengine kuja kuwekeza.

“Tusiweke ruzuku halafu mbolea tukaenda kuagiza nje. Kwanza  kiwe ni kile kinachopatikana ndani ya nchi halafu kinachobakia ndipo mfikirie nje ya nchi ili kulinda wawekezaji wa ndani na kuhimiza wengi kuwekeza kwenye uzalishaji wa mbolea,” alisema.

Aliwahimiza wawekezaji wakubwa kuwekeza Dodoma kutokana na kuwa na eneo kubwa la uwekezaji.

Naye msimamizi wa ujenzi wa kiwanda hicho, Msafiri Dieudonne, alisema kiwanda hicho kimekamilika kwa asilimia 80 na Mwezi Julai mwaka huu kitaanza uzalishaji kwa awamu ya kwanza.

"Bei ya mbolea itakuwa chini ili kupunguza gharama na wanaofanya hesabu wameshaanza kufanya na mwisho wa mwezi Agosti watatoa majibu,"alisema.

Awali, Meneja kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Abubakar Ndwata, alisema kiwanda hicho kitatoa ajira za moja kwa moja kwa watu 3,000 na kuwataka watanzania kuchangamkia fursa za uwapo wa kiwanda hicho.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, alimpongeza mwekezaji wa kiwanda hicho ambaye ni raia wa Burundi kwa kuwekeza mkoani Dodoma jambo ambalo alisema  litaondoa dhana iliyopo kwa watu kuwa Mkoa huo ni wa shughuli za serikali pekee.

Habari Kubwa