CCM, Ukawa waungana kugomea bajeti nyeti

17May 2018
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
CCM, Ukawa waungana kugomea bajeti nyeti

WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana waliungana na wabunge wa upinzani bungeni kuikataa bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka ujao wa fedha.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba kwenye viwanja vya Bunge.

Dalili za kutoungwa mkono kwa bajeti hiyo ya Sh. bilioni 170.2, zilianza kuonekana juzi, wabunge walipoanza kuchangia mjadala wa kuipitisha baada ya Waziri Charles Tizeba kuiwasilisha.

Wabunge wengi waliochangia juzi walisema haiakisi hali halisi ya sekta ya kilimo nchini kisha jana kukaibuka hoja ya kuitaka serikali iiondoe bungeni ili ikajipange upya na kuiwasilisha ikiwa na mikakati bora ya kuimarisha sekta hiyo muhimu.

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), alisema kuna kila sababu bajeti hiyo kuondolewa bungeni, akieleza kuwa idadi kubwa ya wabunge walioichangia kabla yake hawakuiunga mkono.

“Katika michango ya wabunge wa pande zote mbili, wengi wao hawaungi mkono bajeti hii, Nape alisema, "kama ni suala la maendeleo ya watu, bajeti hii ndiyo inagusa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania.

"Na kelele tunazosikia kwenye pamba na kwenye mazao mengine ni kwa sababu sekta hii inagusa maisha ya watu moja kwa moja.

“Lakini, bado tunayo nafasi ya ujumbe tunaotaka kuupeleka kwenye umma, kwamba tunajali nini kati ya maendeleo ya vitu au maendeleo ya watu ambao ndiyo waliotuweka madarakani?

“Ukiangalia ‘trend’ ya mwaka 2016/17, utaona serikali ilitenga asilimia 0.93 kwenye bajeti kwa ajili ya Wizara ya Kilimo, bajeti ya mwaka 2017/18 ikashuka hadi asilimia 0.85 na katika mapendekezo ya sasa hivi, tumeshuka tena hadi kwenye asilimia 0.52 ya bajeti yote.

“Hii maana yake ni kwamba kila mwaka tunashusha bajeti tunayotenga kwenye sekta inayogusa watu zaidi ya asilimia 80 kuliko sekta nyingine.

“Kwa hiyo, ushauri wangu katika hili, serikali isione aibu kuipitia upya bajeti hii kwani tukiipitisha kama ilivyo, ujumbe kwa Watanzania ni mbaya sana kwa serikali ya awamu ya tano na itaonyesha tunataka kuwekeza zaidi kwenye vitu badala ya watu.

“Nikiikubali bajeti hii, wananchi wakulima wa korosho, mbaazi, ufuta, pamba na wengineo, watanishangaa.“Pamoja na hayo, naangalia Ilani ya CCM ambayo baadhi yetu hawataki tuinukuu, naona inapingana na bajeti hii. Kwa hiyo, tuishauri serikali irudi mezani, iende ikaipitie upya na kuweka vipaumbele vya wananchi."

Nape pia alihoji matumizi ya fedha zinazokusanywa na serikali, akieleza kuwa anashangaa kuona bajeti haitekelezwi ilhali serikali inabana matumizi na mianya yote ya ufujaji wa fedha za umma na mapato yake yameongezeka.

Mbunge huyo wa CCM pia alieleza kutoridhishwa na vipaumbele vya serikali kwa kile alichodai kuwa serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika miradi mikubwa inayoweza kujiendesha yenyewe na kushindwa kuwekeza fedha za kutosha katika miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), aliunga mkono hoja ya Nape kutaka bajeti hiyo iondolewe bungeni kupitia Kanuni ya 69 ya Bunge ili kutoa nafasi kwa Waziri wa Kilimo na Waziri wa Fedha na Mipango kukaa na kuona jinsi ya kuiboresha.

“Sisi wabunge, hasa wa CCM, tuna wajibu wa kuwalinda wakulima wakiwamo wa mahindi, pamba, wafugaji wa ng’ombe na wavuvi wa samaki, lakini sisi ndiyo tunaowanyanyasa," Bashe alisema.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu amempa binadamu utu na akili ya kuwajali wenzake, lakini sisi tunawanyanyasa wenzetu. Kwa kuwa bajeti hii imetengewa fedha kidogo, nashauri tuirudishe ili ikaandaliwe upya."Mbunge huyo wa chama tawala pia alieleza jinsi wakulima wanavyotumia gharama kubwa katika kilimo lakini wanapata fedha kidogo wakati wa mauzo.

Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Hilaly Aeshi (CCM), aliungana na wabunge wenzake hao na kuitaka serikali kuiondoa bajeti hiyo bungeni ili ikaandaliwe upya na kuwasilishwa tena kwa kuwa Bunge la Bajeti bado lina muda wa kutosha.

Aeshi alishauri wakulima waruhusiwe kuuza mazao yao popote wanapotaka na serikali ilipe madeni ya mawakala wa pembejeo za kilimo kwa kuwa baadhi yao wameanza kupoteza maisha kutokana na madeni wanayodaiwa. 

Alieleza baadhi ya mawakala wanaoidai serikali zaidi ya Sh. bilioni 60 , wiki hii wamekuwa wakifika bungeni kuzungumzia na mawaziri na wabunge lakini wengi wao wana hali mbaya kifedha na wamegeuka kuwa ombaomba kwa watunga sheria.Wakati Nape, Bashe na Aeshi wakitaka ikitumike Kanuni ya 69 ya Bunge kuiondoa bajeti ya Wizara ya Kilimo bungeni, Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge (CCM), alipinga hoja hiyo akiwaomba wabunge wenzake wakubaliane naye itumike Kanuni ya 105 ya Bunge ili bajeti hiyo ipitishwe lakini hoja zao za msingi zichukuliwe na Kamati ya Bajeti ambayo itajadiliana na serikali jinsi ya kuiboresha.

Alisema haoni haja bajeti hiyo kuondolewa bungeni badala yake wazipe muda mamlaka husika kwa kutumia Kanuni hiyo ya 105 ya Bunge kujadili maeneo yaliyolalamikiwa kabla ya bajeti kuu kuwasilishwa.

Pamoja na hilo, Chenge pia alipinga utaratibu wa serikali kutumia vyama vya ushirika kununua mazao na badala yake akataka utumike utaratibu mwingine.Mbunge wa Karatu, Willy Qambalo (Chadema), alisema Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, hana tofauti na Waziri Kivuli ambaye huwa hana fedha za kuendeshea wizara.

Alisema jambo pekee linalomtofautisha waziri huyo na Waziri Kivuli ni kwamba yeye anapewa gari la serikali.

Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema), aliungana na wabunge wa CCM waliotaka bajeti hiyo kuondolewa bungeni akisema kuwa serikali haiwezi kufanikiwa katika suala la viwanda kwa sababu imeshindwa kuimarisha sekta ya kilimo.

Naye Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF), alisema Tanzania kutenga Sh. bilioni 170.2 kwa ajili ya bajeti ya Wizara ya Kilimo hakuakisi mpango wa kuwa na nchi ya viwanda.

Kutokana na hali hiyo, alisema sera ya Tanzania ya viwanda haitawezekana kama serikali haitaongeza fedha katika sekta ya kilimo.

Mbunge huyo wa CUF pia alipendekeza alama ya jembe la mkono kwenye bendera ya CCM iondolewe kwa sababu imepitwa na wakati kwa kuwa nchi sasa inahitaji kilimo cha kisasa na si kilimo cha jembe la mkono lililopo katika bendera hiyo.

Mtolea pia alisema kuna mchezo mchafu unafanyika kwenye kilimo cha miwa kwa lengo la kuwabeba wazalishaji wakubwa wa sukari nchini.

Kwa upande wake, Mbunge wa Morogoro Vijiji, Omary Mgumba (CCM), aliipongeza serikali kwa kuondoa zuio la kuuza mahindi nje ya nchi, akieleza kuwa imetoa imetoa fursa kwa wakulima.

Hata hivyo, mbunge huyo alisema kwa sasa Morogoro bado haijawa tayari kuuza mazao kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa kuwa mpaka sasa hakuna hata kikao kimoja kilichofanyika kupitia suala hilo mkoani humo na hakuna maghala na vyama vya wakulima. 

Habari Kubwa