CCM: Wagombea ruksa kujipitisha

01Jul 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
CCM: Wagombea ruksa kujipitisha

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimefungua pazia kwa wanaotaka kuwania nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kuanza kujipitisha kwenye maeneo wanayotaka kugombea kuanzia leo, lakini kipenga rasmi cha uchukuaji fomu kitapulizwa Julai 14 mwaka huu.

Katibu wa CCM, Dk. Bashiru Ali, picha mtandao

Hata hivyo, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli amewataka wanachama wenzake kutotumia kipindi hicho cha kampeni kukibomoa chama chao, akisisitiza kuwa wavumilivu.

Akizungumza na wanachama wa CCM waliojitokeza alipokuwa akirejesha fomu za kuwania urais kupitia chama hicho jijini Dodoma jana, Rais Magufuli alisema kuanzia leo, wanaCCM ruksa kupitapita kwenye maeneo.

"Ninawaomba wanaCCM kwa upendo mkubwa sana, wale tutakaojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za udiwani, ubunge, uwakilishi, tufanye hizi kazi kwa ustaarabu, tukatangulize maslahi ya Tanzania yetu, maslahi pia ya chama chetu.

"Katika kipindi hiki cha kampeni, wanaCCM kamwe tusikitumie kama kipindi cha kukibomoa chama, kwa sababu tutakwenda kule tutaanza kubomoana wenyewe kwa wenyewe.

“Wakati utakapofika sasa wa uchaguzi na kugombea na vyama vingine tutakuwa tumeshajiumiza. Niwaombe sana wanaCCM tukawe wavumilivu, ninaambiwa majimbo mengine kuna watia nia hadi 25, mtarogana bure, mtaumizana bure atakayechaguliwa Mungu anamjua.

“Tuvumiliane, tuheshimiane, tupendane na baada ya uchaguzi, huyo atakayekuwa amechaguliwa, ndiyo tumbebe kwa nguvu zote,” aliagiza.

Pia aliviomba vyama vingine vya siasa kuwateua wanawake, vijana na wazee kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

“Tanzania ina umuhimu zaidi kuliko mengine, na ninataka niwathibitishie mambo yanakwenda vizuri, vizuri sana na kila mahali ukigusa, unaona kuna miradi inafanyika.. Hatujali hawa hawakutuchagua, tuliamini kila Mtanzania anahitaji maendeleo," alisema.

AREJESHA FOMU

Dk. Magufuli alisema Juni 17, mwaka huu, alichukua fomu na alitaka uchukuaji wake uwe wa kawaida akifafanua: “Niliamini kabisa uchukuaji fomu wangu uwe kama kawaida yangu, nilijitahidi kuwatoroka vizuri sana, Katibu Mkuu alikuwa ananiuliza nitakuja lini, alipanga na saa tano na saa sita mimi nikaja saa mbili nikachukua fomu nikaondoka.

“Lakini, nilifika jana Katibu Mkuu, Makamu Mwenyekiti na viongozi wengine wamekuwa wakiniuliza unarudisha lini fomu uliyoijaza, ndiyo maana leo nimerudisha fomu, kwa kutambua kwamba mimi ni mtumishi wenu, na inawezekana bado mnanihitaji nitumike,”alisema.

“Ninaomba radhi kwa waliotaka kunidhamini, lakini karatasi hazikutosha, dhamana yao sasa waiweke katika kura zao na kwa wanachama wengine wa vyama vyote, ikiwa nitapitishwa na mikutano inayohusika kuwa mgombea wa urais,” alisema.

Katibu wa CCM, Dk. Bashiru Ali, alisema wanachama 1,023,111 wamejitokeza kumdhamini Dk. Magufuli kuwania urais kupitia chama hicho.

Alisema uchukuaji na urejeshaji wa fomu za urais wa Tanzania na Zanzibar ulitarajiwa kufungwa rasmi jana saa 10 jioni na kuthibitisha kupokea fomu za Rais ambazo zimejazwa vizuri na amekamilisha taratibu za kuomba nafasi hiyo.

“Julai 11, mwaka huu kutakuwa na mkutano utafanyika Dodoma ili kupiga kura kwa mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, ili ateuliwe rasmi na kwa Zanzibar Julai 10 Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) itampigia kura na kuchagua mgombea urais mmoja wa CCM,” alisema.

Alisema kuanzia leo nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani zipo wazi, hivyo wanachama walio na sifa, waanze kupita kwenye ofisi za wakurugenzi wa uchaguzi kuulizia utaratibu na siyo kuanza kampeni.

“Kwa wagombea nafasi hizo Julai 14 hadi 17 watachukua na kurejesha fomu. Kwa hiyo, hicho kipindi cha kuanzia kesho (leo) ni cha kujipitishapitisha na siyo cha kufanya kampeni.

"Atakayekiuka kanuni, Mzee Mangula yupo hapa na mimi nipo nyuma yake, tunahitaji ushindani wenye utulivu, wa kistaarabu, wa kiCCM na matarajio tutapata wagombea wazuri wa kushindana na vyama vingine,” alisema.

Habari Kubwa