CCM yaahidi furaha kwa wajasiriamali

11Sep 2020
Gwamaka Alipipi
GEITA
Nipashe
CCM yaahidi furaha kwa wajasiriamali

​​​​​​​CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025, kimewaahidi kuwanyanyua zaidi vijana, wanawake na makundi ya wajasiriamali kwa kuwapatia mafunzo, stadi za ujasiriamali, usimamizi wa shughuli za kiuchumi na kuwawezesha kurasimisha shughuli zao.

Dk. John Magufuli.

Katika ukurasa wa 24 wa ilani hiyo ambayo inanadiwa na mgombea wa urais kupitia chama hicho, Dk. John Magufuli, kunabainisha kuwa serikali chini ya chama hicho itaanzisha utaratibu wa kuwakopesha vifaa na mitaji wanafunzi wanaohitimu mafunzo ya ufundi nchini kwa masharti nafuu.

Vilevile, chama hicho kimewahakikishia wananchi kuwekewa mazingira mazuri ili kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mbali na hayo, chama hicho pia kimeweka mkakati wa kuimarisha viwanda nchini, kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vipya vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo, samaki na rasilimali nyingine za maji kwa kutumia taasisi za umma, sekta binafsi na vikundi vilivyosajiliwa na vyama vya ushirika.

Pia, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, chama hicho kimepanga kuanzisha vituo vya uendelezaji wajasiriamali kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwawezesha wananchi kupata ithibati za kimataifa ili kupanua wigo wa fursa za ajira na biashara.

Kwenye Ilani hiyo, CCM pia imepanga kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi shirikishi kwa kutoa fursa kwa wananchi wote pamoja na kuinua hali ya maisha.

Katika kipindi cha miaka mitano ijayo chama hicho kimepanga kuanzisha kanzidata ya watoa huduma katika miradi mikubwa ya kimkakati na kutoa elimu kwa umma juu ya ushiriki wa wajasiriamali katika miradi hiyo.

“Kanzidata hii itawezesha kuunganisha sekta binafsi na wawekezaji au wakandarasi na hivyo kuwawezesha kupata masoko ya bidhaa zao na kufanya kazi kwa ubia na kampuni za nje ili kukuza ujuzi na kuhaulisha teknolojia," inabainishwa katika ilani hiyo.

Kuhusu ujenzi wa viwanda, CCM imepanga kujenga ukanda na kongani za viwanda kila mkoa, kulingana mazao na maliasili zinazopatikana katika kila mkoa na fursa za kijiografia kwa mkoa husika.

Vilevile, kinatarajia kuimarisha mazingira ya ujenzi wa viwanda vya kimkakati kwa kufanya mapitio na maboresho ya sera na mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kutekeleza mpango kazi wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Katika ilani hiyo, viwanda hivyo vimetajwa kuwa ni pamoja na vile vinavyotumia teknolojia itakayotoa ajira kwa watu wengi, lengo likiwa ni kuongeza ajira zitokanazo na uzalishaji wa bidhaa viwandani kutoka 306,180 mwaka huu hadi 500,000 mwaka 2025.

Chama hicho pia kimepanga serikali yake kuendeleza na kujenga viwanda mama vikiwamo vya chuma, dawa na kemikali, ambavyo vitaleta faida nyingi kwa taifa kama vile ajira na uongezaji thamani malighafi za ndani.

Habari Kubwa