CCM yaitaka Wizara ya Nishati kumaliza kero kukatika umeme

17Sep 2021
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
CCM yaitaka Wizara ya Nishati kumaliza kero kukatika umeme

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza Wizara ya Nishati kuhakikisha inatafuta suluhu ya kukatika kwa umeme kila wakati nchini ikiwamo katika Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka, alitoa agizo hilo juzi wakati akizungumza na wananchi wa shina namba moja la Nambambo na shina namba mbili la Namatula ambao walimlalamikia kuwapo kwa tatizo la kukatika kwa umeme kila wakati na hata vifaa vyao kuungua pamoja na ubovu wa barabara.

Shaka alisema hawataweza kuvumilia changamoto za kuwaumiza wananchi na ndiyo maana wameamua kufanya ziara katika mashina ili kuwakumbusha viongozi wajibu wao katika kutatua kero za wananchi.

 

“Hatutamvumilia mtumishi yeyote ambaye amepewa dhamana na serikali yetu halafu yeye akafanya vile ambavyo anataka yeye, chama hakitamvulimia na ndiyo maana tumekuja kuwasikiliza na kuwauliza viongozi wana mipango gani,” alisema Shaka.

“Nimepewa taarifa hapa kuna mama kajinyima kanunua jokofu lake sasa hivi limekufa kwa umeme kukatika mara kwa mara, hapa tunawasaidia wananchi ama tunawarudisha nyuma.”

Katika kushughulikia tatizo hilo, Shaka alimpigia simu Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato na kuiweka sauti yake wazi kwa wananchi (loud speaker) ili wamsikie na kumuuliza ni lini atatatua tatizo hilo la kukatika umeme kila wakati katika wilaya hiyo.

Byabato alisema wanaendelea kusimamia na kutekeleza yale ambayo wameyaahidi kwenye Ilani ya CCM.

Alisema walikuwa na kikao cha kufuatilia kwa nini siku za hivi karibuni kumekuwa na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.

“Maelezo yaliyo mengi ni miundombinu kuchakaa na shughuli nyingine za kibinadamu kukata miti, kuchoma moto na kingine ni urekebishaji wa miundombinu wamekuwa hawatoe taarifa ninakuomba kiongozi jambo hilo tumekubaliana kufanya kikao cha ndani kutafuta suluhu mwanzoni mwa wiki ijayo nitatoa taarifa,” alisema.

Shaka alisema chama hakiwezi kupita katika maeneo na kusikia vilio vya wananchi ambao ukiangalia kwa kiasi kikubwa badala ya kusonga mbele wanarudi nyuma.

“Chama kinaelekeza mje na majibu na kutueleza ni lini wanamaliza tatizo hili ili wananchi wapate maendeleo badala ya kuwarudisha nyuma,” alisema Shaka.

Shaka alisema ziara hiyo imelenga kuhamasisha na kuimarisha uhai wa chama kuanzia ngazi ya shina, kuhimiza uhusiano ndani ya chama na serikali.

Shaka ameendelea kuwahakikishia wananchi kuwa CCM na serikali ipo salama na imara katika mikono ya Mwenyekiti na Rais Samia Suluhu Hassan na amejipanga kuleta maendeleo makubwa katika nchi.

"Hii ni kwa sababu katika muda mfupi serikali anayoiongoza imetoa mwelekeo wenye matumaini makubwa ya kuimarisha ustawi wa wananchi, uchumi wa nchi yetu, kuvutia uwekezaji zaidi, kuzalisha ajira kwa vijana na kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi yetu na raia wote," alisema Shaka.

Shaka amewataka viongozi na watendaji wote ndani ya serikali kuchapakazi kwa kuwa chama, Rais Samia na wananchi wanataka matokeo yanayoonekana na yanayopimika kutoka kwenye utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025.