CCM yajipanga kushinda umeya Dar kwa nguvu

27Feb 2016
Beatrice Shayo
Dar
Nipashe
CCM yajipanga kushinda umeya Dar kwa nguvu

WAKATI uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es Salaam ukitarajia kufanyika leo, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vikiongozwa na Chadema vimelalamikia uwezekano mkubwa wa kuchezewa rafu katika uchaguzi huo.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu.

Vyama hivyo vimesema CCM imeandaa mazingira ya kushinda kwa gharama yoyote na tayari wameshapata taarifa za vurugu zitakazosababisha baadhi ya wapiga kura wa Ukawa kutolewe nje ya ukumbi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, alisema CCM wameandaa mbinu chafu ambazo zimepangwa ili kuwahujumu kwenye uchaguzi huo.

Alisema kwa takwimu zilizopo, Ukawa ina wajumbe wengi kuliko CCM hivyo hakuna sababu zozote za kuufanya upinzani ushindwe kuliongoza Jiji hilo.

Alisema wamebaini mbinu ambazo CCM na serikali inakusudia kuzitumia hasa kutumia Jeshi la Polisi na vifaa vyake kuhujumu uchaguzi huo jambo ambalo hawatakubaliana nalo.

“Wanataka kutumia Jeshi la Polisi kutuhujumu, wanataka kututisha kwa namna yoyote ile ndani ya ukumbi ili tukifanya fujo watolewe madiwani au wabunge wetu ili tupungue, tumeshajua na tumejipanga lazima haki itendeke,” alisema Mwalimu.

Alisema kuwa wanataka kuutumia uchaguzi huo kama ule wa Umeya wa Tanga, aliposhinda wa Ukawa lakini Mkurungenzi aliamua kutumia nguvu zake kumtangaza wa CCM ambaye alishindwa.

Hata hivyo, alisema madiwani na wabunge wa Ukawa wako tayari kwa uchaguzi huo ambao umeahirishwa mara mbili na leo wanatarajia kuweka historia.

Naye Mkuu wa Idara ya Mawasiliano Chadema, Tumaini Makene alisema chama chake kimejipanga kwa ushindi na kwamba hawatishiki na vurugu za kutengeneza zilizoandaliwa na serikali.

Alisema kuna njama zimepangwa ili madiwani wao wakamatwe, hatua ambayo itaipa ushindi CCM lakini alisema wamejipanga kukabiliana na ujanja wowote ambao umepangwa kufanyika.

Pia alisema kuna mpango wa kuvunjwa kwa Halmashauri ya Jiji ili kuandaa Tume ya Jiji ambayo itakuwa inaendeshwa na serikali.

Makene alisema Chadema na Ukawa hawatakubaliana na ubabaishaji huo kwasababu serikali imekua ikiahirisha uchaguzi huo ikiandaa mazingira ya kulazimisha ishinde.

Uchaguzi huo ambao ulipangwa kufanyika Januari 23 mwaka huu, uliahirishwa bila kutolewa sababu za kueleweka.
Idadi ya wapinzani wanaotarajiwa kupiga kura ni 87 na CCM wakiwa 74.

Vyama vilipatiwa barua ya kuahirishwa kwa uchaguzi bila kuelezwa sababu za kuahirishwa kwa uchaguzi huo wa Umeya.

Habari Kubwa