CCM yajisifu utekelezaji miradi Arusha kwa asilimia 90

18Nov 2019
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe
CCM yajisifu utekelezaji miradi Arusha kwa asilimia 90

CHAMA cha Mapinduzi CCM, kimesema kimeridhishwa na utekelezaji ya miradi ya maendeleo mkoani wa Arusha kwa zaidi ya asilimia 90.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole.

Akizungumza na Waandishi wa habari wakati wa kutoa tathimini ya  utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2015/19, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema chama hicho kimeridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa kipindi cha miaka minne.

Polepole, amesema hayo leo katika kikao kazi cha siku mbili kilichofanyika mkoani hapa, ambapo amesema chama hicho kimefanya mambo makubwa ndani ya mkoa wa Arusha.

Amesema wakati chama hicho, kikifanya tathimini ya utekelezaji wa Ilani waliangalia zaidi utekelezaji wa miradi maendeleo katika sekta ya afya, maji, elimu, mifugo, kilimo na ujenzi wa miundombinu ya barabara. 

Amesema mtaji mkubwa wa chama hicho, kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ni chama kuisimamia serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kwa vitendo na siyo maneno ya propaganda.

 "Kazi ya chama ni kuisimamia serikali, kutoa maoni kwa serikali, kutoa maelekezo  kwa serikali na hadi sasa maelekezo hayo yamefanyiwa kazi kwa zaidi ya asilimia 90," amesema Polepole.

Akizungumzia suala la kujitoa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwa baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani, Polepole amesema siyo kweli kwamba vyama hivyo vimejitoa katika uchaguzi bali wameona wananchi hawataweza kuwachagua kutokana na maendeleo yaliyofanywa na serikali kwa kipindi cha miaka minne.

“Kuna baadhi ya vyama vya siasa vimesema vimejitoa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, siyo kwamba wamejitoa bali wameona kutokana na maendeleo ya kasi yaliyofanywa na serikali kwa kipindi cha miaka minne wemeona wananchi hawawezi kupotenda muda wa kuwapigia kura,”amesema Polepole na kuongeaza kuwa;

“Vipo vyama vya siasa vinasema vimejitoa kwenye uchaguzi wakati hawana hata wanachama, ukiangalia kwa Mkoa wa Arusha vyama vilivyosema vimejitoa wagombea waliochukua fomu na kuzirudisha ni wachache mno na waliopitishwa kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu hawazidi 10,”amesema Polepole.

Katika hatua nyingine Polepole ametoa onyo kwa vyama vya upinzani ambavyo vimedai wananchi wasubiri kupewa maelekezo endapo uchaguzi huo utafanyika. 

"Tunaomba vyama vya upinzani wasitujaribu tunaomba jeshi la polisi kama kukiwepo kwa matukio ya uvunjia wa amani katika uchaguzi sheria ichukuwe mkondo wake,"amesema Polepole.

Aidha amesema chama hicho, katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwenye vijiji na vitongoji , kimepita bila kupingwa kwenye baadhi ya maeneo ambayo uchaguzi utafanyika wamejipanga kushinda.

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM  Mkoa wa Arusha, Gerald Munisi, amesema katika Mkoa wa Arusha wilaya zote zimefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa hospitali, vituo vya afya, zahanati, miradi ya maji na ujenzi wa madarasa katika shule za msingi na sekondari.

Aidha amesema kwa Jiji la Arusha kuna ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wa sh.bilioni 520, unaendelea na upo katika hatua za mwisho kukamikika.

"Wilaya za Longido,Karatu, Monduli, Ngorongoro na Arumeru serikali imepeleka huduma ya ujenzi wa miradi ya maji, miundombinu ya barabara na miundombinu ya elimu.Katika sekta ya afya serikali imejenga vituo vya afya vya wilaya vitano kwa kila wilaya za Karatu,Longido, Monduli, Ngorongoro, Arumeru na Jiji la Arusha," amesema 

Amesema kabla ya serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani katika mkoa wa Arusha kulikuwa na hospitali mbili za wilaya.

Kwa upande wa Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha Mussa Matoroka, amesema kutokana na maendeleo yaliyofanywa na chama hicho, kushinda katika chaguzi zote.

Amesema kwenye maeneo ambayo uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika watakwenda kuwaeleza wananchi mambo yaliofanywa na serikali kwa kipindi cha miaka minne tangu kuingia madarakani.

"Tutakwenda kuwaeleza wananchi tuliahidi nini na tumeshafanya nini hadi muda huu kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, Mtaa, kata, wilaya, mkoa mpaka taifa,"amesema Matoroka.

Amesema katika uchaguzi wa mwaka 2015,  mkoa wa Arusha ulifanya vibaya kwa kutoa kura nyingi kwa vyma vya upinzani, lakini bado serikali hiyo, iliendelea kuwajali wananchi kwa kupeleka miradi mikubwa ya maendeleo, hivyo taswira ya awali imewabadilika na wamekubali kuiunga mkono serikali.

Habari Kubwa