CCM yajivunia kufanya kampeni za kisayansi

12Sep 2020
Gwamaka Alipipi
Chato
Nipashe
CCM yajivunia kufanya kampeni za kisayansi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kinajivunia kufanya kampeni zake za uchaguzi mkuu kisayansi, kikitamba kuwa hadi kufikia Oktoba 27, mwaka huu, kitakuwa kimekifikia kila kijiji nchini.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey
Polepole, akizungumza na waandishi wa habari mjini Chato, Mkoa wa Geita, jana. PICHA: IKULU

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole, aliwaambia waandishi wa habari Chato mkoani Geita jana kuwa CCM kwa sasa inafanya kampeni za kisayansi na weledi wa hali ya juu kwa kujigawa katika makundi yanayoshambulia kila kona ya nchi.

Polepole alikuwa akizungumzia tathmini ya siku 10 za mwanzo za kampeni za chama hicho, akidai kuwa wamebaini endapo uchaguzi mkuu ukifanyika sasa, mgombea urais kupitia chama hicho, Dk. John Magufuli ataibuka mshindi kwa asilimia 85.

Alisema hadi sasa Dk. Magufuli ameshafanya kampeni katika mikoa minane, mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan, ameshafika mikoa ya nyanda za juu, kusini na kati, akitumia usafiri wa barabara na kufanikiwa kufika kila kijiji.

Alisema mjumbe wa kamati kuu, Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu, ameshashambulia mikoa ya Dodoma, Manyara na Arusha wakati viongozi wengine akiwamo Rais mstaafu Jakaya Kikwete wakifanya kampeni mikoa ya kusini, huku mjumbe mwingine wa kamati kuu, Mizengo Pinda na Spika Job Ndugai, wakishambulia mikoa ya kanda ya kati.

“Hadi ifikapo Oktoba 27, mwaka huu (siku moja kabla ya uchaguzi), tutakuwa tumefika kila kijiji, kila kata, kila kitongoji, kila mkoa tutakuwa tumefika, tumejigawa na tunashambulia kila kona,” alitamba Polepole.

Polepole alisema CCM ina kitengo cha utafiti ambacho kimekuwa kikishirikiana na vitengo vinginevyo na kwamba Februari kiliwahoji wananchi 4,998 na kupata matokeo ya asilimia 90 ya ushindi kwa Dk. Magufuli.

Alisema kuwa katika utafiti wa kisayansi walioufanya, endapo uchaguzi ungefanyika mwezi huu, CCM ingeshinda kwa asilimia 75 upande wa wabunge na asilimia 85 kwa madiwani.

“Tutaimaliza nchi hii awamu hii yote, kisha tutapiga awamu nyingine, na kisha tutapiga awamu nyingine. Kwa sasa tumejiimarisha, wanachama tulionao kwa sasa ni milioni 17," alitamba.

Polepole pia alijibu hoja ya wapinzani wao kisiasa kuhusu serikali kutoongeza mishahara kwa watumishi wa umma, akisema kuwa tangu Dk. Magufuli aingie madarakani Novemba 5, 2015, hakujawahi kutokea mfumuko wa bei.

"Rais amedhibiti mfumuko wa bei, amewafutia kodi wafanyakazi ambao mishahara yao haizidi Sh. 300,000, kodi kwa watumishi wa umma ilikuwa tarakimu mbili na sasa imeshuka hadi tarakimu moja, amefanikiwa kuweka nidhamu katika matumizi pamoja na kuongeza makusanyo," alisema.

Alisema kwenye nyanja ya diplomasia, Dk. Magufuli alipoingia madarakani na kupewa uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), alisimamia nidhamu na matumizi na baadaye aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Nchi Kusini mwa Afrika (SADC) na kufanikiwa kukipigania lugha ya Kiswahili na kuimarisha Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

“Sasa hivi dawa zote za SADC zinatoka MSD, MSD imeshonwa, imeimarishwa vizuri, nidhamu iko juu na hiyo ndiyo imesababisha kuendelea kuwa kinara katika ukanda huu. Kwa hiyo, nitoe rai ifikapo Oktoba 28, mwaka huu, Watanzania wakamchague Dk. Magufuli kwa maendeleo ya Tanzania,” alisema Polepole.

Kuhusu hoja ya wapinzani wao kwamba wananchi wanafurika kwenye mikutano ya kampeni za CCM kwenda kuona wasanii na wengine kupelekwa kwa magari maalum, Polepole alisema:

"Mikutano yetu inakuwa na malengo mawili, kwanza tunasherehekea mafaniko ya miaka mitano pamoja na kuomba kura, hapo tunatumia wasanii kufikisha ujumbe kwa sanaa, pili tunaomba dhamana ya muhula wa pili.

"Watu wanakuja kwenye mikutano yetu kwa kujitegemea kwa usafiri na wengine wanakuja kwa miguu."

Habari Kubwa