CCM yampitisha Dk. Tulia kugombea uspika wa Bunge

21Jan 2022
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
CCM yampitisha Dk. Tulia kugombea uspika wa Bunge

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC-NEC), imempitisha Dk. Tulia Ackson kuwa mgombea wa nafasi ya Spika wa Bunge.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kikao hicho, Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alisema Dk. Tulia amepitishwa kwa ajili ya kwenda kupambana na wagombea wa vyama vingine watakaopitishwa.

Shaka alisema baada ya Kamati Kuu kuchambua na kujadili kwa kina, imeamua kumteua Dk. Tulia kuwania nafasi hiyo.

Wabunge wanatarajia kukutana Januari 31, mwaka huu, kwa ajili ya kumpigia kura mgombea huyo ili aende kupambana na wagombea kutoka katika vyama vingine.

Alisema Kamati Kuu haina shaka na uteuzi wa Dk. Tulia ambaye atakwenda kuiwakilisha CCM kuwania nafasi hiyo iliyoachwa na Job Ndugai baada ya kujiuzulu mapema mwaka huu.

Shaka aliishukuru Kamati Kuu kwa kazi nzuri iliyoifanya katika kikao hicho, wanampongeza kwa kuteuliwa huko.

Alibainisha kuwa kikao hicho chini ya Mwenyekiti Rais Samia Suluhu Hassan, kimefanyika kwa weledi na kuchambua
majina na hatimaye kumpitisha Dk. Tulia na kazi anayoifanya kwa Watanzania wenzake.

Katika hatua nyingine, Shaka alisema Kamati Kuu imempongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kutokana na kusimamia uchumi wa bluu kwa ufasaha. Shaka alisema Kamati Kuu imeridhishwa na utendaji huo.

WADAU WAPONGEZA

Kutokana na uteuzi wa Dk. Tulia, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga, alisema amepokea kwa furaha uamuzi huo na ana matumaini kuwa atakuwa spika mzuri kwa kuwa ana uzoefu wa kutosha.

“Nilikuwa na imani kuwa atashinda kutokana na uzoefu wake lakini nimefurahi zaidi kuona kuwa ile agenda yetu ya wanawake ya 50/50 ya kuwa na wanawake wawili katika mihimili mitatu ya dola itakuwa imetimia.

Alisema anatarajia bunge litakuwa  zuri japokuwa halitakuwa na mabadiliko sana na lililopita kutokana na kutokuwa na uwakilishi wakutosha kutoka vyama pinzani.

Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. George Kahangwa, alisema uzoefu katika kazi ya uspika na usomi wake katika sheria na ndivyo vimempa nafasi kubwa ya kuteuliwa kugombea kiti hicho.

“Kama tunavyofahamu yeye ndiye alikuwa naibu spika, kwa hivyo kama atachaguliwa kuwa Spika atakuwa anakwenda kwenye ofisi anayoijua na ninategemea kuwa usomi wake utalisaidia taifa,” alisema.

Habari Kubwa