CCM yataja siri wagombea wake kutoenguliwa NEC

21Oct 2020
Thobias Mwanakatwe
Dar es Salaam
Nipashe
CCM yataja siri wagombea wake kutoenguliwa NEC

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimefichua siri kuhusu wagombea wake kutoenguliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kigezo cha kushindwa kujaza fomu.

Aliyefichua siri hiyo ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally, katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la BBC, jana alfajiri kuhusiana na mambo mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu.

Dk. Bashiru  alipoulizwa suala la wagombea wengi wa ubunge na udiwani wa upinzani kuenguliwa na NEC na je, CCM ilitumia mbinu gani hadi wagombea wake hata mmoja asienguliwe? Alijibu kuwa siyo suala la mbinu, bali ni suala la kutii na kufuata sheria hasa ikizingatia kuwa uchaguzi nchi zote unasimamiwa na sheria na kanuni.

"Zipo sheria zinazoelekeza namna gani vyama vifanye uteuzi kupitia kwenye mifumo yao ya vyama, viombe uteuzi NEC, namna gani wagombea wake wajaze fomu, muda wa kuchukua na kurejesha fomu," alisema.

Dk. Bashiru alisema kwa upande wa CCM vipo vitengo vya sheria vinavyosimamia na kuruhusu wagombea wa ngazi zote kujaza fomu na kisha kuhakikiwa.

Katika mchakato wa wagombea wa udiwani na ubunge Agosti mwaka huu, NEC iliwaengua wagombea wengi wa upinzani kwa maelezo ya kukiuka masharti ya ujazaji wa fomu.

Hali hiyo ilisababisha CCM ipate wabunge 28 ambao wamepita bila kupingwa, na kwa sasa wanasubiri kuapishwa, baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.

Hata hivyo, wagombea ubunge na udiwani kupitia upinzani walioenguliwa walikata rufani NEC, ambayo kwa awamu tofauti iliwarejesha baadhi ya walioshinda rufani kuanza kampeni.

Katika hatua nyingine, CCM imelitaka Jeshi la Polisi kuzingatia mafunzo yao na weledi na kutumia nguvu zisizopindukia kiwango katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Dk. Bashiru, alisema hayo alipoulizwa kuwa kumekuwa na hali ya usalama kuteteleka hususani maeneo ambako wapinzani wanafanyia kampeni, polisi wanatumia nguvu kupita kiasi.

Akijibu alisema: "Wito wangu  ni jukumu la polisi kuzingatia mafunzo yao na weledi na kutumia nguvu zisizopindukia kiwango.”

Hata hivyo, Dk. Bashiru alisema katika kipindi hiki wananchi wahakikishe wanatii sheria bila shuruti kwa sababu polisi wana mafunzo ambayo yanawafanya watathmini hali ilivyo na kuchukua hatua.

 

"Wapo wagombea wanajua sheria, mwisho wa kufanya kampeni ni saa 12:00 jioni,  hiyo siyo sheria ngeni, lakini unakuta mgombea anafanya mkutano na wafuasi wake saa 2:00 usiku,” alisema.

Alisema tabia za namna hiyo za kuvunja kanuni za maadili ya uchaguzi zitaweza kuwa chanzo cha matatizo kama hayo.

Dk. Bashiru akijibu swali aliloulizwa kwamba wapo baadhi ya watu wanajisikia kutokuwa huru nchini,

alisema hakuna mahali popote uhuru ukawa ni shibe iliyokamilika, kila nchi  duniani kuna madai ya upeo wa uhuru, hivyo hakuna jamii itatosheka na uhuru huo.

"Uhuru ni kama njaa ambayo kila ukila unahitaji kula zaidi na kama ni lishe yako inahitaji kuboreshwa ili kuongeza virutubisho,” alisema.

 

Habari Kubwa