CCM yatia neno muswada vyama

17Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
CCM yatia neno muswada vyama

VIONGOZI na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamekutana kujadili na kutoa maoni kuhusu muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, PICHA NA MTANDAO

Katika maoni yao, wengi wameonyesha kuunga mkono muswada huo hasa vipengele vinavyompa nafasi msajili wa vyama vya siasa kujua mapato na matumizi ikiwamo ruzuku.  Pia wametaka hatua ya kuruhusiwa vyama kuungana isiwekewe mipaka. 


Muswada huo uliowasilishwa bungeni Novemba, mwaka jana jijini Dodoma, umepokewa kwa namna tofauti kwa kuwa baadhi ya vyama vya upinzani, hasa vyenye wabunge vimeonyesha kuupinga. 

Akifungua mkutano huo, Katibu wa  Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Kanali (mstaafu) Ngemela Lubinga, alisema ni jukumu la vyama kuhakikisha vinatoa maoni ya kuboresha muswada huo ili kuwasaidia wanachama na wananchi kwa ujumla.

Lubinga alisema pamoja na mambo mengine, muswada huo unapiga marufuku kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi na usalama ndani ya vyama vya siasa jambo ambalo ni sahihi, kwa kuwa kazi ya jeshi ni kulinda na kuhakikisha serikali iliyopo madarakani inaongoza kwa msingi wa haki na kuzingatia sheria.
 
“Mabadiliko ni juhudi za kuwaweka wananchi katika hali nzuri. Msajili wa vyama vya siasa kazi  yake kubwa anayofanya ni kwenda na hitaji la Watanzania. Wenzetu wanavyouawa ni fundisho kwamba kila unachokifanya unatakiwa kuwa makini,” alisema Kanali Lubinga.  

“Wanatuletea fedha kuwa ziendeshe mafunzo ya siasa, lakini wapo waovu leo hii viwanda vya silaha ndiyo vina faida kubwa kuliko vile vinavyotengeneza vitu vya matumizi ya kijamii. Tanzania hatujachukua nusu ya bajeti yetu kununua silaha, hawajafurahi kwa sababu waliona hapa ndipo kwenye keki,” alisema.

Pia alisema kutokana na hali ya mazingira ilivyo watendaji wa serikali wenye dhamana wako makini kupitia mfumo na kuchambua, huku wakitumia njia ya demokrasia kwa kupeleka bungeni kwa ajili ya kujadiliwa kisha ndipo utumike.

“Hatua hii ni kutengeneza mazingira kwenda na hali ya mahitaji ambayo yamechanganyika, hivyo busara zaidi inahitajika kutumika. Dhamana tuliyopewa leo hii watu ni wajeuri kwa sababu wanashiba, taasisi zetu wenye dhamana ya kuendesha serikali saa zote zinaandaa utaratibu wa kuepusha shari,” alisema.

Alisema CCM iliposhinda uchaguzi mwaka 2015, ilichukua madaraka lakini kuna watu hawakufurahishwa.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema wameamua kutumia vyema nafasi iliyotolewa na bunge ya kutoa maoni kuhusu muswada huo, ambapo pia viongozi wa vyama tisa vya upinzani waliudhuria kushuhudia mjadala huo.
 
Alisema sheria inayotumika sasa ina mambo kadhaa yanayotakiwa kufanyiwa marekebisho, ikiwamo kumpa nafasi nzuri msajili wa vyama vya siasa kuvisimamia na kuhoji vyama hivyo.   
 
“Msajili anatakiwa awe huru kuhoji kuhusu vyama vyetu ikiwamo vikao vilivyoketi kupitisha wagombea, kwa sasa mamlaka hayo hana na atapata ikiwa muswada huu utapitishwa kuwa sheria,” amesema Polepole.

 

Habari Kubwa