CCM yawaonya ma-RC, ma-DC

15May 2022
Na Mwandishi Wetu
Babati
Nipashe Jumapili
CCM yawaonya ma-RC, ma-DC

​​​​​​​KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka, amesema kuna ukimya kwa wakuu wa mikoa na wilaya katika kuelezea mafanikio ya serikali.

​​​​​​​KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka.

Shaka alisema hayo jana mjini Babati mkoani Manyara katika mkutano wa ndani wa kujitambulisha mbele ya wanachama wa CCM kama mlezi mpya wa chama hicho akichukua nafasi ya Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.

“Wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya kote nchini mna jukumu la kuyaeleza mafanikio ya serikali ya Mama Samia, sasa hivi kuko kimya hammtendei haki Rais wetu," alionya.

Shaka alisema kuwa katika utafiti alioufanya, miaka miwili iliyopita kila mkuu wa mkoa na wilaya alikuwa akitoa taarifa za mafanikio ya serikali, jambo ambalo ni tofauti na hali ilivyo sasa.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wake, Rais Samia amefanya makubwa kana kwamba amekaa miaka mitano, ikiwamo kuifungua Tanzania kiuchumi na kidiplomasia.

“Rais Samia ni kinara wa demokrasia katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, hili liko wazi. Lazima tuyaseme mafanikio hayo," alisema Shaka aliyekuwa anazungumza kwa ukali.

Alisema kuwa Rais Samia toka aingie madarakani, amechukua hatua kadhaa za kulainisha uhasama na kuponya vidonda.

Habari Kubwa