CCM yazindua awamu ya tatu kampeni

28Sep 2020
Thobias Mwanakatwe
Dodoma
Nipashe
CCM yazindua awamu ya tatu kampeni

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimezindua awamu ya tatu ya kampeni huku kikisema hakitakuwa tayari kujibu uchonganisha unaofanywa na wapinzani wao badala yake kimejipanga kuwashinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Bashiru Ally, akizungumza jana wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Jimbo la Kongwa, mkoani Dodoma, alisema uchaguzi wa mwaka huu ni wa aina yake kutokana na CCM kushindana na watu waliochoka kisiasa.

"Dawa yao si kuwapuuza ni kuwashinda ili wachague njia tatu, mojawapo ama kuja CCM na tutawapokea kwa sababu ni wenzetu au kustaafu siasa na kuanza kujenga upya vyama vya kitaasisi vitakavyoshindana na CCM," alisema.

Dk. Bashiru alisema, CCM viongozi wamegawana kanda katika kupiga kampeni na kushawishi wananchi wajitokeze kwa wingi katika kupiga kura siku ya Oktoba 28, mwaka huu.

"Makisio yetu hadi leo (jana) CCM ina uhakika wa kushinda kwa zaidi ya asilimia 89 kwa nafasi ya urais, wabunge na madiwani," alisema.

Alisema kwa wastani kila siku madiwani, wabunge na wawakilishi wa CCM wanafanya mikutano ya kampeni 600 wakati kampeni za kitaifa zinazoongozwa na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli na viongozi wengine wanafanya wastani wa mikutano 20 kwa siku.

Kwaupande wake mgombea mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alisema ikiwa wananchi watakipa ridhaa chama hicho, kimejipanga kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kukamilisha iliyobaki.

Mama Samia alisema kwa Mkoa wa Dodoma miongoni mwa miradi itakayotekelezwa ni ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato ambao kazi ya usanifu ilishakamilika na inayofuata ni kutafuta mkandarasi ili ujenzi uanze mara moja.

Alisema miaka mitano ijayo, wananchi wakiichagua, Serikali ya CCM, itawakopesha vifaa wanafunzi wanaomaliza vyuo vya ufundi kwa masharti nafuu ili waweze kujiajiri na wao kuajiri wenzao.

Alisema kutaanzishwa programu maalum kwa wanafunzi watakaomaliza elimu ya vyuo vya juu kupatiwa mitaji ili waweze kuanzisha miradi na kujiajiri wenyewe.

Habari Kubwa