CHADEMA, RC wapimana ubavu

21Jul 2021
Richard Makore
MWANZA
Nipashe
CHADEMA, RC wapimana ubavu

SIKU moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutangaza kufanya kongamano la kudai Katiba Mpya jijini Mwanza leo, Mkuu wa Mkoa huo, Robert Gabriel, amepiga marufuku mikusanyiko isiyo ya lazima ili kujikinga na ugonjwa wa corona.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Gabriel alisema mikusanyiko isiyo ya lazima ikiwamo sherehe haitakiwi.

Hata hivyo, alisema nyumba za ibada zinaruhusiwa kuendelea na ibada, lakini waumini wote waendelee kuchukua hadhari ikiwamo kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka.

Alisema serikali imeshaanza mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona na sasa imefanya maboresho ili kuhakikisha wanalipa mkazo suala hilo.

Alisisitiza suala la elimu ikiwamo uvaaji wa barakoa ili kuzuia kuambukiza wengine na mtu mmoja mmoja kujikinga.

Wakati kiongozi huyo wa mkoa akitoa agizo hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), John Pambalu, amesisitiza kwamba mkutano wao wa leo utafanyika kama ulivyopangwa.

Alisema jana kuwa wamechukua tahadhari ikiwamo kuvaa barakoa ili kuhakikisha wanajikinga na ugonjwa wa corona.

Juzi, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema jijini Mwanza kuwa tatizo la corona ni kubwa, lakini hatua zinazochukuliwa na serikali zimekuwa hafifu kwa kuwa hakuna bajeti yoyote iliyotengwa kwa ajili ya kupambana nalo.

Alisema gharama ya kumhudumia mgonjwa mmoja katika hospitali za kawaida kwa wiki zinafikia Sh. milioni 2.5 huku hospitali za binafsi zikitoza mpaka Sh. milioni 15 kwa mgonjwa mmoja.

Mbowe alisema ugonjwa wa corona ni janga la dunia na kwamba serikali ilitakiwa kulichukulia hivyo na kuweka mikakati na bajeti ya kutosha badala ya kuendelea kufanya alichokiita mizaha.

Habari Kubwa