Chadema haina mpango wa kuwawekea dhamana waliokamatwa

18Jul 2021
Richard Makore
Mwanza
Nipashe Jumapili
Chadema haina mpango wa kuwawekea dhamana waliokamatwa

​​​​​​​KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida,  Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema hakina mpango wa kuwawekea dhamana viongozi wake waliokamatwa juzi na Jeshi la Polisi  jijini  Mwanza.

Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana la Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA),  John Pambalu.

Chama hicho kimesema kwa sasa kinajiandaa na mkutano mwingine wa kudai katiba mpya, baada ya Polisi jijini Mwanza kuvunja kikao chao na kuwakamata viongozi mbalimbali wa chama hicho mwishoni mwa wiki  iliyopita.

Juzi viongozi 38 wa Chadema walikamatwa jijini Mwanza muda mfupi kabla ya kuanza mkutano wa kudai katiba mpya na kushikiliwa katika vituo vya polisi vya Kirumba na Kati mkoani humo.

Akizungumzia sakata la kukamatwa viongozi hao, Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana la Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA),  John Pambalu, amesema, hawawezi kuwawekea dhamana kwa kuwa hawajui kosa la viongozi hao.

Pambalu amesema Polisi wao wakitaka kukaa nao ni sawa na kama wakitaka kuwafikisha mahakama watajua wao, lakini  chama hicho hakiwezi kwenda kuwadhamini.

Ameongeza kuwa kwa sasa wanachokifanya Chadema ni kuwapelekea chakuka viongozi hao waliopo mahabusu za polisi.

Pambalu ambaye anaongoza harakati hizo za kudai katiba jijini Mwanza amesema polisi wana hamu ya kukaa na viongozi hao mahabusu na kwamba wao  waendelee kukaa  nao.

"Viongozi hawa hawana kosa lolote, lakini kwa kuwa polisi wana hamu ya kukaa nao mahabusu wacha waendelee kufanya hivyo na  kama wataamua kuwafikisha mahakamani pia watajua wao,''  amesema Pambalu

Ameongeza kuwa wao kwa sasa kama BAVICHA wanaendelea na maandalizi ya kikao kingine cha kudai katiba mpya ambacho kitafanyika wiki hii jijini Mwanza, lakini siyo kuhangaika kuwawekea dhamana viongozi waliokamatwa kwa kuonewa.

Amesema  Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe anatarajia kushiriki katika mkutano huo wa kudai katiba mpya wiki hii jijini Mwanza.

Hata hivyo, amesema taarifa kamili itatolewa kuhusu ujio wa mwenyekiti huyo na ushiriki wake wa mkutano wa kudai katiba mpya.

Habari Kubwa