Chadema sasa ni 'Kata Funua'

29Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
MTWARA
Nipashe
Chadema sasa ni 'Kata Funua'

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kinajiandaa kuja na operesheni mpya yenye jina la ‘Kata Funua’, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuingia katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2019.

Agosti mwaka huu, Chadema ilitangaza operesheni Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) ambayo ilikuwa ikihamasisha
maandamano ya Septemba Mosi, ambayo hayakufanyika hata hivyo.

Operesheni Kata Funua ilitangazwa jana na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, wakati akihitimisha mkutano wa ndani wa chama hicho uliowahusisha viongozi wakuu wa chama wilayani Masasi mkoani Mtwara.

Mbowe alisema kwamba kwa sasa chama chake kinazunguka kwa kuigawa nchi katika kanda 10 na pindi watakapomaliza kutembelea kanda hizo, ndipo wataanza Kata Funua.

“Viongozi wakuu wa chama kwa maana ya kamati kuu ya chama, wameshatembelea kanda ya kati yenye mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro, Kanda ya Nyasa yenye mikoa ya Iringa na Mbeya na sasa hivi wako katika kanda ya kusini yenye mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma," alisema Mbowe.

"Baadaye tunajipanga kutembelea Kanda ya Ziwa, Kanda ya Magharibi na kanda zingine, ambazo ziko kisiwani Zanzibar na tukimaliza kuzungukia kanda zote, tutaanza na operesheni mpya ya Kata Funua.”

Akifafanua operesheni hiyo, Mbowe alisema itahusisha madiwani na wabunge kwa kufanya mikutano kwa kila kata kwa ajili ya kuzungumza na wananchi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 na baadaye uchaguzi mkuu mwaka 2020.

“Katika operesheni yetu mpya ya Kata Funua, madiwani na wabunge wa chama chetu kwa umoja wao watakuwa wakienda kila kata na kila kanda kwa ajili ya kuongea na wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla,” alisema.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chadema kwa upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu, alisema chama bado kiko imara kwa kuwa wamejionea katika kanda tatu ambazo wameshatembelea na kukuta wanachama bado wana moyo na wanaamini kinaweza uwezo wa kuchukua dola katika chaguzi zingine zijazo.

“Katazo la kutokufanya siasa mpaka 2020 limezidi kutuimarisha zaidi. Awali tulikuwa tunatembelea zaidi wananchi kupitia mikutano ya hadhara, lakini sasa katazo hilo limetupa fursa ya kufanya mikutano ya ndani na tumekutana na wanachama wengi zaidi,” alisema Mwalimu.

Awali akizungumza katika mkutano huo wa ndani, aliyekuwa mgombea wa Urais kupitia Chadema na kuungwa mkono na vyama vilivyokuwa vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, aliwashukuru wananchi wa kanda ya kusini kwa kumpa kura nyingi ingawa hakushinda.

“Natumia fursa hii ya mkutano huu wa ndani kuwashukuru wananchi wote wa kusini kwa kunipa kura nyingi licha ya kuwa sikuweza kuibuka mshindi,” alisema Lowassa huku akikumbushia baadhi ya wanasiasa walivyoponda afya yake, lakini baadhi yao wamefariki dunia.

Habari Kubwa