Chadema wamjibu Spika hatima ubunge wa Lissu

21Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Chadema wamjibu Spika hatima ubunge wa Lissu

SIKU moja baada ya Spika Job Ndugai kumtaka Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kurejea nchini, uongozi wa chama chake umekosoa uamuzi huo na kusisitiza utapigania haki zake.

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema.

Juzi, Spika Ndugai alikaririwa na vyombo vya habari akimtaka mbunge huyo kurejea nchini ili kuendelea na shughuli za Bunge kwa kuwa hana kibali cha kuwa nje ya nchi.

Ndugai alikaririwa akisema Lissu hana ruhusa ya kuwa nje ya Bunge, hivyo anatakiwa kurejea nchini kuendelea na shughuli za ubunge.

Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alikosoa agizo hilo la Spika Ndugai, akieleza kuwa anayeweza kuthibitisha kupona kwa Lissu ni madaktari wanaomtibu.

Mrema alisema kuwa mpaka sasa, hakuna anayejua Lissu amepona ama la.

“Yeye (Spika) si daktari mpaka aseme kuwa Lissu amepona na hajawahi kumtembelea kwa kipindi chote tokea apelekwe hospitali," alisema Mrema na kuongeza:

“Tunakumbuka aliyewahi kuwa waziri wakati wa serikali ya awamu ya nne, Prof. Mark Mwandosya aliugua kwa zaidi ya mwaka, lakini hatukusikia kauli za aina hii."

Alipoulizwa na Nipashe kwa nini Lissu ameanza kutembelea nchi kama Uingereza, aliyoitembelea wiki iliyopita, ilhali bado ni mgonjwa, Mrema alisema Ubelgiji na Uingereza si mbali kwa kuwa ni saa moja tu kwa usafiri wa ndege.

Akizungumzia suala la kile kinachodaiwa njama za kutaka kumvua ubunge Lissu, Mrema alidai zimeshavuja kabla ya kutekelezwa huku akisisitiza kuwa hazitafanikiwa.

“Hiyo ni njama ambayo imeivuja na tuimeinasa kabla haijatekelezwa na itashindwa kama zilivyoshindwa njama zingine,” alidai Mrema.

Kwa zaidi ya mwaka, Lissu amekuwa Ubelgiji akipatiwa matibabu ya kibingwa kutokana na kupigwa risasi na watu wasiojulikana alipokuwa anajiandaa kushuka kwenye gari nyumbani kwake Area D Septemba 7, 2017 mchana alipokuwa anatoka kushiriki kikao cha Bunge.

Baada ya shambulio hilo, mbunge huyo aliwahishwa kwenye Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma, alikopatiwa matibabu ya awali kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya na baadaye kupelekwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

Habari Kubwa