CHADEMA wataka uchunguzi waliochoma ofisi zao Arusha

15Aug 2020
Na Waandishi Wetu
Arusha
Nipashe
CHADEMA wataka uchunguzi waliochoma ofisi zao Arusha

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitaka serikali kuwakamata wahalifu waliochoma ofisi ya chama hicho Kanda ya Kaskazini.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, ofisi hizo zilizoko jijini Arusha, zilichomwa moto usiku wa kuamkia jana na kusababisha uharibifu wa samani zilizokuwamo na miundombinu ya jengo la ofisi hizo.

Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Benson Kagaila, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa, tukio hilo lilitokea majira ya kati ya saa nane na saa tisa usiku.

Kigaila alidai majirani wa ofisi hiyo walisikia kelele za mlinzi wa ofisi hizo akiomba msaada na baadaye sauti hiyo ilipotea.

Alisema mlinzi wa ofisi hiyo ambaye alidaiwa kutekwa, amepatikana.

"Walioliona jengo, wanasema lilimwagiwa petroli na kuchomwa moto, tunajiuliza sababu ni nini na kwanini ifanyike hivyo," Kigaila alisema.

Aliongeza kuwa, iwapo serikali haitawapata ndani ya siku tano waliohusika na tukio hilo, CHADEMA itawatafuta na kushughulika nao.

“Wanalenga kutisha watu ili waogope kwenda kwenye mikutano, kwenda kudhamini mgombea urais, hatutatishwa, chama hakijafa na kina nguvu kuliko ilivyokuwa zamani, kwenye uchaguzi huu tunakwenda sawa," alidai.

KAULI YA POLISI

Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha, Salum Hamduni, alithibitisha kuteketezwa kwa moto kwa ofisi hizo majira ya usiku wa kuamkia jana.

"Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, lakini tukio lenyewe lilitokea majira ya saa tisa usiku katika ofisi hizo zilizoko katika eneo la Kimandolu jijini.

"Niwaombe wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hili, ili kubaini waliochoma moto ofisi za CHADEMA ili kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Vitu vilivyoteketea ni viti, mito ya makochi, ambayo yalikuwa kwenye baraza la nyumba hiyo na kuvunjwa vioo vya madirisha sita ya nyumba hiyo. Jambo hili tunalichunguza ili kubaini wahusika kwa ajili ya kuwafikisha katika vyombo vya sheria," alisema.

Kamanda Hamduni alisema kuwa hadi wakati huo, hapakuwa na mtu aliyekamtwa kuhusiana na tukio hilo, akiahidi kutoa taarifa kwa vyombo vya habari baada ya vyombo vya dola kukamilisha uchunguzi wake.

Kuhusu madai ya kutekwa kwa mlinzi, Kamanda Hamduni alisema Jeshi la Polisi halikuwa na taarifa juu ya suala hilo.

Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Reginald Masawe, alisema wamesikitishwa na tukio hilo, lakini hakuwa tayari kulizungumzia zaidi, akiacha jukumu hilo kwa uongozi wa chama kitaifa.

“Baada ya kufanya tathimini ya vitu vyote vilivyoteketea, viongozi wetu watazungumza kwenye ngazi hiyo, ila siyo mimi, imetusikitisha sana tukio hili ambalo limetokea wakati tunampokea Makamu Mwenyekiti wetu wa taifa, Tundu Lissu," alisema.

Licha ya kutokea kwa kuchomwa kwa ofisi hizo, umati mkubwa wa watu ulijitokeza jana kwenye eneo hilo kumdhamini Lissu aliyechukua fomu kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuomba kuteuliwa kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.

*Imeandikwa na Romana Mallya (DAR) na Daniel Sabuni (ARUSHA)

Habari Kubwa