Chadema: Waumini wasali nyumbani

24Mar 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Chadema: Waumini wasali nyumbani

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeshauri viongozi wa dini kuruhusu waumini wao kufanya ibada nyumbani ili kuepusha msongamano kutokana na tishio lililopo la ugonjwa wa corona.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Freeman Mbowe alipozungumza na Waandishi wa Habari kwenye Ofisi za Kanda ya Kati za Chama hicho zilizopo eneo la Area C Jijini Dodoma leo, kushoto ni Mwenyekiti wa Kanda ya Kati wa Chama hicho ,Lazaro Nyalandu

Vilevile, kimesitisha mikutano yake iliyokuwa ianze Aprili 4 mwaka huu kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo unaoitesa dunia kwa sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, alisema kutokana na mikusanyiko kuzuiwa, si vibaya viongozi hao wakachukua tahadhari kuruhusu waumini kufanya ibada nyumbani.

“Viongozi wetu wa kiroho washauri watu kufanya ibada nyumbani, tuchukue tahadhari kila njia wala tusipuuze, hatujasema Watanzania waache kumwomba Mungu atuepushe na hili janga.

"Kama mikusanyiko ni kichocheo cha huu ugonjwa, basi mikusanyiko yote ni tatizo ikiwamo nyumba za ibada, katika masoko yetu, tutafute namna bora ya kukabiliana nao,” alisema.

Mbowe alisema wako tayari kushirikiana na serikali na Watanzania katika kukabiliana na ugonjwa huo, huku akiwataka viongozi mbalimbali kutoa ushirikiano kwa jamii inayowazunguka kwa kila hatua inayotolewa na wataalamu.

“Chama chetu tuwe wa kwanza kuonyesha kwa mfano, hatutakuwa na mikutano tuliyopanga kuifanya hadi hapo hali ya nchi itakapotengamaa upande wa ugonjwa huu wa corona,” alisema.

Mbowe alisema siku chache zilizopita baada ya kutoka gerezani na kabla serikali haijatoa taarifa kuhusu mlipuko wa ugonjwa huo, yeye alitoa maelekezo kwa chama hicho kuanza mikutano ya hadhara Aprili 4 mwaka huu.

“Lengo la mikutano hiyo ni kuzungumzia kuhusu kuwapo tume huru ya uchaguzi na chama kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

"Tangu nimetoa kauli, idadi ya washukiwa wa ugonjwa huo imeongeze na kuwa 12, jambo linaloonyesha kuwa mlipuko ni mkubwa hivyo wananchi na wanachama wachukue tahadhari kukabiliana nalo maana si la kupuuza,” alisema.

Mbowe alisema janga la corona si la kupuuza kwa kuwa serikali imesimamisha shughuli mbalimbali na kufunga baadhi ya shughuli zake.

Kuhusu bajeti, alishauri bajeti maalum kwa ajili ya corona iwekwe badala ya kusubiriwa fedha za Mwenge ndiyo zitumike.

Alisema ni vyema kuwa na fungu maalum kabla ya kusubiri Bunge la Bajeti likae ndiyo itenge fedha, bali itenge na kuwatangazia Watanzania imejiandaaje.

“Tunatambua hatua ngumu zilizochukuliwa zina athari, lakini serikali iongeze 'awareness' (uelewa) ya corona, vyombo vya habari vyote vitoe elimu na isikubaliane na kauli ya kwamba wananchi wanatishwa,” alisema.

Alisema hatua ya serikali kusema kuwa kipimo kifanyike Dar es Salaam pekee si sawa na badala yake viwekwe nchi nzima ili huduma hiyo ipatikane kwa urahisi wanapotokea wenye ugonjwa huo.

“Serikali itenge bajeti maalum au itoe bajeti maalum na si kutegemea fedha za mbio za Mwenge zisaidie kutibu corona, tunataka maandalizi ya kutosha, hospitali zetu za mikoa na wilaya ziwe ni kituo cha kupima na kutoa huduma kwa wagonjwa mbalimbali,” alisema.

Mbali na hilo, Mbowe alisema serikali itafakari kama ni sahihi kuacha mipaka wazi na watu kuendelea kuingia licha ya kuwa nchi nyingine zimechukua tahadhari kwa kufunga mipaka.

“Serikali itafakari kwa makini kuhusu kufunga mipaka, tusisubiri watu kuanza kufa kama kuku, Kenya na nchi nyingine zimechukua tahadhari, lakini sijui sisi tunasubiri nini,” alihoji.

Habari Kubwa