CHADEMA wazuiwa kuingia gerezani kumwona Mbowe

24Oct 2021
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
CHADEMA wazuiwa kuingia gerezani kumwona Mbowe

BAADHI ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wamedai kuzuiwa kumwona Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ambaye yuko mahabusu kwenye Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam.

Nipashe ilipomtafuta kwa njia ya simu jana, Mkuu wa Gereza Kuu Ukonga jijini Dar es Salaam, Hamis Lissu, kuhusiana na madai hayo, aliahidi kufuatilia taarifa hizo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na chama hicho kupitia Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema, waliodai kuzuiwa ni pamoja na John Heche, Julius Mwita, wagombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kutoka majimbo mbalimbali nchini na baadhi ya wanachama wa CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam.

“Walipokwenda magereza leo (jana) kwa ajili ya kumsalimia Mwenyekiti Mbowe, walizuiliwa kumwona kwa sababu ambazo magereza walisema, ‘wamepokea maelekezo kutoka juu kuwa wanaoruhusiwa ni wenye vibali tu’.

"Siku za mwisho wa wiki na sikukuu ni siku ya kutembelea wafungwa na mahabusi,” alisema.

Alisema wenye vibali wanaweza kwenda siku yoyote kama ambavyo mawakili hufanya hivyo.

“Waliomba kumwona mkuu wa gereza ila hawakufanikiwa kwa hoja kwamba yuko kwenye kikao, na hivyo wamekaa pale mpaka mchana huu walipolazimika kuondoka bila kufanikiwa kumwona na kujua ana hali gani kiafya,” Mrema alisema katika taarifa yake hiyo.

Alisema wanaendelea kuchukua hatua  mbalimbali ili wajue Mbowe ana hali gani kwa sababu siyo kawaida kwa magereza kuzuia watu kumwona mahabusi au mfungwa isipokuwa kama mtu huyo ni mgonjwa mahututi.

Habari Kubwa