CHADEMA yafafanua ugombea urais Lissu

03Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
CHADEMA yafafanua ugombea urais Lissu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetoa ufafanua kuhusu Makamu Mwenyekiti, Tundu Lissu, kukabiliwa na kesi mahakamani na iwapo atateuliwa kugombea nafasi ya urais kwa tiketi ya chama hicho, kuwa watazungumza na mawakili wao jinsi ya kumsaidia katika kesi zake ili suala hilo..

lisiingiliane na ratiba za kampeni.

Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam baada ya kikao cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyama vya siasa uchaguzi mkuu, Naibu Katibu Mkuu CHADEMA (Bara), Singo Kigaila, alisema Lissu ni miongoni mwa watia nia saba kiti cha urais kupitia chama hicho.

Lissu alirejea nchini wiki iliyopita akitokea Brussels nchini Ubelgiji, alikokuwa amekwenda kwa matibabu tangu Januari mwaka 2018, baada ya kushambuliwa kwa risasi akiwa nyumbani kwake Dodoma.

Kigaila alisema mchakato wa kumpitisha mgombea kiti cha urais ulianza jana baada ya Kamati Kuu kukaa na leo Baraza Kuu litakutana na Mkutano Mkuu unaotarajiwa kufanyika kesho.

"Kesi haiwezi kumzuia mtu kugombea, kuwa na kesi bado ni mtuhumiwa hajahukumiwa," alifafanua.

Alisema kesi haiwezi kumzuia mtu kwenda kwenye kampeni za uchaguzi mkuu kwa sababu hazipo kila siku.

"Tunajua zipo kesi zinazomkabili mahakamani na kama ikatokea akateuliwa kuwa mgombea kiti cha urais, mawakili wataona namna gani ifanyike kuhusu hizo kesi.

"Kwa vyovyote vile inabidi hakimu au jaji aelewe kuna mtu anagombea urais au ubunge ikiwezekana kesi isimame ili akimaliza kampeni ziendelee."

Kuhusu mkutano huo wa NEC na vyama vya siasa alisema eneo la vipeperushi au mabango ili vitumike ni lazima vipate kwanza idhini kwa Tume au wasimamizi wa uchaguzi ama wasaidizi wa wasimamizi wa uchaguzi lina tatizo.

"Tunaona hili suala ni baya kwa sababu hakuna kanuni, sheria au maelekezo yaliyotolewa kwa watakaofanya maamuzi hayo, watakaoidhinisha watafuata misingi ipi, tunaona hili litaleta shida na Tume itabadilika kuwa tatizo badala ya wawezeshaji," alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga, akitolea ufafanuzi kuhusu suala hilo, alisema sheria inasema sifa za mgombea asiwe na hatia ya kukwepa kodi.

"Sheria haisemi lolote kuhusu kuahirisha makosa yanayomkabili mgombea. Kwa hiyo kama kuna haja ya kuahirisha utaratibu wa kawaida wa kuahirisha mashauri utatumika," alisema.

Katika kikao hicho cha Tume na vyama vya siasa, Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Rufani mstaafu, Semistocles Kaijage, alisema daftari la wapigakura lina wapigakura milioni 29,188,347.

Alisema bajeti inayotarajiwa kutumika katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu ni Sh. bilioni 331.7.
Alisema kutakuwa na vituo 80,155 vya kupigia kura na kila kimoja kitakuwa na wapiga kura wasiozidi 500.

Alisema jumla ya asasi za kiraia 97 zenye nia ya kuwa watazamaji wa uchaguzi ndizo zimekidhi vigezo na tayari zimepewa taarifa na zinasubiri kupewa vibali wakati ukifika.

Habari Kubwa