Chadema yamezea mate majimbo Dodoma

13Jan 2020
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Chadema yamezea mate majimbo Dodoma

MWENYEKITI wa Kanda ya Kati wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Lazaro Nyalandu, amesema moja ya zawadi ambayo wanataka kuwapa wanachama wao ni kushinda viti vyote vya ubunge Mkoa wa Dodoma.

Aidha, amesema anatambua kuwa mkoa huo hauna historia ya wabunge wa upinzani kushinda ili kuishangaza CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Nyalandu ambaye amewahi kuwa waziri na mbunge katika serikali ya awamu ya nne, ameiomba serikali kuhakikisha kuna kuwa na tume huru ya uchaguzi ili kila chama kishinde kwa haki, na si kurudia mambo yaliyofanywa katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Nyalandu alisema moja ya mikakati Chadema iliyojiwekea ni kuhakikisha wanashinda makao makuu ambapo viongozi wote wa chama tawala na serikali wapo.

Alisema moja ya mbinu ambazo watazitumia ni kuwa na wanachama wengi, na kwamba wameshawaandikisha watu wao wote katika daftari la kudumu la wapigakura.

"Kuna njia nyingi ambazo tutatumia ili tushinde uchaguzi ujao… hatuwezi kuzisema zote kwa sababu tutawarahisishia wapinzani wetu CCM,” alisema Nyalandu.

Alisema Dodoma ni kubwa, lakini kwa mikakati waliyopanga lazima washinde kwa kishindo, huku wakiwataka CCM kutohofia chochote bali wakutane ulingoni kugombea viti mbalimbali katika uchaguzi huo.

"Naviomba vyombo vya ulinzi na usalama visiingilie mambo ya siasa, wao wafanye kazi yao nasi tutaheshimu sheria za nchi zilizowekwa, hakuna atakayekwenda kinyume,” alisema Nyalandu.

Alisema Chadema imejipanga kuichukua Dodoma kwa sababu ni sehemu ya mkakati waliojiwekea.

"Tulitembea nyumba hadi nyumba eneo la Ikoje, huku tukiwasemesha Kinyaturu, lakini baada ya matokeo tulipigwa na kupoteza lile jimbo,” alisema Nyalandu.

Akizunguzia suala la kuhamia Chadema, Nyalandu, alisema alikaa nalo mwaka mmoja ndipo siku moja alimwambia mke wake ambaye alishtuka na kushangazwa na uamuzi huo.

"Naomba niwaambie kuhama kwangu CCM sio upepo wa kisulisuli, mafuriko wala nguvu ya soda bali hii ni nguvu ya ‘wine’, kadri siku zinavyoendelea ndio inazidi kuwa bora nami sibahatishi, nimedhamiria,” alieleza.

MIKOPO ELIMU YA JUU

Akizungumzia suala la elimu kwa ujumla, alisema serikali inapaswa kubadilisha mfumo haraka kwani unawagharimu sana wanafunzi wa elimu ya juu hususani suala la mikopo.

"Haiwezekani mwanafunzi anadai haki yake ya mkopo unamsimamisha chuo au kumfukuza hiyo roho ya ukatili Tanzania haipo mweleweshe, lakini kumtoa chuo unamwaharibia malengo na hujui watu wangapi wako nyuma yake wanamtegemea,” alisema Nyalandu.

Habari Kubwa