Chadema yampoteza Dk. Mahanga

24Mar 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Chadema yampoteza Dk. Mahanga

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepata pigo baada ya kada wake na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Ilala, Dk. Makongoro Mahanga, kufariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam jana.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii iliyosainiwa na Ofisa habari wa chama hicho Kanda ya Pwani, Lyenda Gervas, kiongozi huyo alifariki saa 12:30 asubuhi katika hospitali hiyo alikokuwa amelazwa tangu Machi 21, mwaka huu.

“Dk. Mahanga amefikwa na mauti akiwa anapata matibabu kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Dk. Mahanga aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana katika Serikali ya awamu ya nne na baadae mwaka 2015, alihamia Chadema.

Aliwahi kuwa mbunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi katika Jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam kwa miaka 10 mfululizo kuanzia mwaka 2000 mpaka 2010, kabla ya jimbo hilo kugawanywa na kupatikana Jimbo la Segerea alikoshika nafasi hiyo kwa miaka mitano.

Mwaka 2015, Dk. Mahanga aligombea tena ubunge kwenye jimbo la Segerea kwa tiketi ya Chadema, lakini aliangushwa na mgombea wa CCM, Bonnah Kamoli, anayeshikilia kiti hicho hadi sasa.

Dk. Mahanga ndiye pekee aliyebaki Chadema miongoni mwa waliokuwa makada wa CCM waliohamia upinzani wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, wengine walikuwa ni mawaziri wakuu wastaafu Edward Lowasa na Fredrick Sumaye.

Pia, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Juma Mwapachu na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Ardhi ,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye ambao wote kwa sasa wamerejea CCM.

Baada ya kuhamia upinzani, Mahanga alikuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa serikali na kuonekana kuwa mtu muhimu katika upinzani, hata hivyo kada huyo alipowania uongozi wa ndani ya chama katika nafasi ya Katibu wa Baraza la Wazee Chadema (Bazecha) alishindwa na mpinzani wake na Katibu wa sasa wa baraza hilo, Rodrick Lutembeka.

Wakati huo huo, Chama cha ACT-wazalendo kimetoa pole kwa Chadema kufuatia kifo cha kada wake, katika taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma, Janeth Rithe, chama hicho kimetoa pole kwa familia na chama kwa ujumla.

Habari Kubwa