CHADEMA yapuliza kipenga Zanzibar

02Jul 2020
Elizaberth Zaya
Zanzibar
Nipashe
CHADEMA yapuliza kipenga Zanzibar

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), kimetoa ratiba ya utaratibu wa kupata wagombea wa urais, uwakilishi na udiwani visiwani Zanzibar huku mgombea urais visiwani humo kupitia chama hicho akitarajiwa kujulikana Julai 29.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana na Ofisi ya Chama hicho Makao Makuu Zanzibar, uchukuaji wa fomu za urais, kutafuta wadhamini na kuzirejesha, utaanza rasmi Julai 4 hadi 19 saa 10 jioni.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa Julai 20, Kamati Maalum itaketi kupitia majina ya wagombea wa nafasi hiyo ya urais na kuwasilisha ripoti yake mbele ya Kamati Kuu.

Pia, Julai 22, Kamati Kuu itapendekeza jina la mgombea au wagombea wa urais na 29 mwezi huo itaketi mkutano mkuu kwa ajili ya kuteua mgombea wa urais wa kupeperusha bendera ya chama hicho.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa wagombea wa nafasi za ubunge na uwakilishi utaanza Julai 4 hadi 10.

Ilielezwa zaidi katika taarifa hiyo kuwa, kura za maoni na uteuzi wa awali wa kamati za utendaji utafanyika Julai 13 hadi 17, wakati Julai 25 Kamati Maalum itafanya uteuzi wa awali wa wagombea wa ubunge na uwakilishi na Julai 30 hadi 31, Kamati Kuu itateua wagombea wa nafasi hizo.

"Julai 11 hadi 17 itakuwa ni kuchukua na kurejesha fomu za udiwani, Julai 20 hadi 23, kura za maoni zitakusanywa na Kamati ya Utendaji Kanda na Julai 24 itakuwa ni kamati za utendaji kuteua wagombea wa nafasi hizo," ilielezwa katika taarifa hiyo.

Kwa upande wa ubunge na uwakilishi viti maalum, taarifa hiyo ilisema kuwa, kuanzia Julai 4 hadi 10, itakuwa ni uchukuaji na urejeshaji, Julai 13 hadi 17 itakuwa ni mahususi kwa kura za maoni na uamuzi wa kamati za utendaji.

Ilieleza kwamba Septemba 14, Kamati Maalum itapitia na kufanya uteuzi wa awali wa wagombea na kuwasilisha ripoti yake mbele ya Kamati Kuu na Julai 14 hadi 25, wagombea wateuliwa.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa ajili ya wagombea wa udiwani viti maalum, utafanyika kuanzia Julai 11 hadi 17, wakati Julai 20 hadi 23 itakuwa ni kura za maoni na kamati za utendaji.

"Kamati Maalum itafanya uteuzi wa awali wa nafasi hiyo za udiwani viti maalum na kuwasilisha ripoti yake mbele ya Kamati Kuu Septemba 14, na Julai 14 hadi 15, Kamati Kuu itateua wagombea wa nafasi hizo.

Habari Kubwa