Chadema yashtukia zengwe uchaguzi wa meya jiji Dar

09Feb 2016
Veronica Assenga
Dar
Nipashe
Chadema yashtukia zengwe uchaguzi wa meya jiji Dar

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemtaka Rais John Magufuli kutenda haki na kuheshimu utawala wa sheria kwenye uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, alisema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), iko chini ya Rais na kwamba inawajibika kwenye uchaguzi huo.

Alisema kuwa Rais anapaswa kuwajibika kwenye masuala mazito na kwamba kwa sasa anakwamisha uchaguzi huo kwa maslahi yake na ya chama chake.

“Rais anatakiwa kusafisha ofisi iliyo chini kwa maana ya Tamisemi na George Simbachawene (Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- Tamisemi) ni kama naibu kwenye wizara hiyo, hivyo sisi tunahitaji Rais atumbue jipu kwenye wizara yake kwa kuanza na kibanzi kilichoko kwenye jicho lake,”alisema.

Mwalimu alisema uchaguzi huo umeahirishwa mara ya pili sasa na kwamba sababu zilizoelezwa na Simbachawene kuwa wanaandaa mfumo wa upatikanaji wa wajumbe kutoka kwenye halmashauri tatu za Jiji la Dar es Salaam, si za kweli.

Alisema kuna wajumbe 14 waliongezwa katika mazingira ya kutatanisha kwa lengo la kushiriki kwenye upigaji kura kumchagua meya wa jiji.

Mwalimu aliwataja wajumbe hao 14 kuwa watatu wanatoka Manispaa ya Ilala na wengine 11 wanatoka Manispaa ya Kinondoni.

Wakati huo huo, chama hicho kimewapongeza wabunge wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kufanya kazi kubwa bungeni ijapokuwa lilitawaliwa na ubabe mkubwa.

“Tunawaasa sasa wabunge wote wa Ukawa kufanya kazi kwa mshikamano ndani ya majimbo yao ili kuleta maendeleo chanya yatakayofuta kauli kwamba chama pinzani hakitaweza kushika dola,” alisema

Aidha, Mwalimu alitumia fursa hiyo kuzungumzia kitendo cha kufutwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya bunge, kuwa kunaonesha serikali ya awamu ya tano ni dhaifu.

“Unapofungia matangazo ya bunge kuonyeshwa moja kwa moja kwa wananchi, inamaanisha kuna kitu kinachofanywa na serikali ambacho unaogopa wananchi kukigundua ,” alisema.

Habari Kubwa