Chadema yaukosoa utaratibu kupitisha maadili uchaguzi 2030

28May 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Chadema yaukosoa utaratibu kupitisha maadili uchaguzi 2030

WAKATI Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikitoa fursa ya siku moja kwa vyama vya siasa kujadili na kupitisha maadili ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeikosoa hatua hiyo.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, PICHA MTANDAO

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alisema haiwezekani itengwe siku moja kujadili na kuisaini bila kutoa muda kufanya marekebisho kama yapo.

“Sheria ilivyo, tume imeweka kwenye maadili haya kifungu ambacho kinatulazimisha hata kama hayapo sawasawa lazima kuyasaini.

“Ni kitu ambacho kimsingi hakikubaliki, lakini kwa sababu wameshakiweka na kama mlivyoona ratiba ya leo ni ya vyama kujadili na kusaini, tutafanya hivyo.”

Alisema tafsiri yake ni kwamba tume imeshafanya uamuzi na leo wameitwa kujadili na kusaini.

Mnyika alisema Chadema itasaini, lakini haimaanishi wanakubaliana na mambo mengine ambayo hayafai kwenye maadili hayo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Democratic Party (DP), Abdul Mluya, alisema awali walipatwa na mshtuko kwa nini wajadili na kusaini, lakini wamebaini hakuna vitu vipya kilichobaidilika ni mpangilio ndio umebadilika hivyo hawaoni sababu ya kutokusaini.

Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria wa Chama cha Wananchi (CUF), Salvatory Magafu, alisema: “Rasimu ipo vizuri na tunakwenda kuipitisha kwa kanuni, kuna mambo mazuri, lakini kuwapo kwa mambo mazuri ni jambo moja na kuyasimamia ni jambo lingine, tunaipitisha iwe kanuni hivyo zinapaswa kusimamiwa kwa maslahi ya wadau wote wa uchaguzi.”

Naye, Mwanasheria wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ernest Makunga, alisema rasimu hiyo inakwenda kutengeneza maadili ya uchaguzi ya rais, wabunge na madiwani na itaweka mazingira bora ya kufanya uchaguzi kuanzia kampeni hadi mwisho.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Rufani mstaafu Semistocles Kaijage, alisema maadili hayo yanapaswa kufuatwa kwa lengo la kudumisha amani ya nchi na kuwa na uchaguzi huru na wa haki.

“Tume imejidhatiti na imejipanda kuhakikisha kuwa inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba, sheria na kanuni pamoja na kuzingatia masharti ya kanuni za maadili ya uchaguzi,” alisema.

Alisema wanaamini serikali, viongozi wa siasa, na wagombea binafsi wataheshimu maadili hayo na kuhamasisha wanachama wao kuyaheshimu.

Mkurugenzi wa NEC, Dk. Wilson Charles, alisema rasimu hiyo imelenga kutatua changamoto zilizojitokeza kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 katika uchaguzi mkuu na zile ndogo zilizofuata baadae.

“Nec ilipitia maoni hayo na kuyafanyika kazi, vyama vitatu ambavyo ni NCCR Mageuzi, Chadema na Alliance for Democratic Change (ADC) viliwasilisha maoni kwa kuchelewa kiasi kwamba tume ilikuwa imeshaleta kwenu barua ya mwaliko wa kikao hiki cha leo,” alisema.

Alivitaja vyama vilivyowasilisha maoni yao kwa wakati Nec ni DP, Tadea, CUF, CCM, CCK, AFP, UPDP, UMD na Chauma.

Habari Kubwa