Chai ya 1,000/- 'yaliza' walimu

16Jan 2017
George Tarimo
IRINGA
Nipashe
Chai ya 1,000/- 'yaliza' walimu

ZAIDI ya walimu 900 kutoka mikoa ya Iringa na Njombe wanaohudhuria mafunzo ya siku nane katika Chuo cha Ualimu Kleruu mjini Iringa, wamegoma kuendelea na mafunzo hayo baada ya kushindwa kukubaliana na malipo ya posho na waandaaji wake na kuuziwa kikombe cha chai Sh. 1,000.

Kwa mujibu wa walimu hao, utaratibu wa malipo ya posho hizo umebadilishwa kutoka ule wa kawaida wa kulipa posho kwa kuzingatia viwango vya mishahara kwa kila mshiriki na badala yake zinalipwa kwa kiwango sawa cha Sh. 60,000 kwa kila mshiriki.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati taofuti, baadhi ya walimu hao walieleza kutokukubaliana na kitendo cha kukatwa Sh. 15,000 kwa ajili ya chai na chakula cha mchana, huku kikombe kimoja cha chai wakiuziwa Sh. 1,000 sawa na bei ya kitafunwa.

"Haiwezekani tuuziwe kikombe cha chai Sh. 1,000. Kweli hii inawezekana katika maisha ya sasa ya Mtanzania? Hata hotelini hatuuziwi hivyo," alisema mmoja wa walimu hao.

Kutokana na kutoridhishwa na bei ya chakula wanachopewa kwenye mafunzo hayo, walimu hao waliomba utaratibu wa chakula ubadilishwe ili kila mshiriki apewe Sh. 15,000 akajitafutie chakula mwenyewe huku wengine wakidai wanao uwezo wa kushiriki mafunzo hayo bila kupata chakula cha asubuhi na mchana.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Taasisi ya Elimu (TEA) ambayo mbali na kulipa posho kwa kiwango sawa kwa kila mshiriki, imedaiwa kumkata kila mshiriki Sh. 15,000 kwa ajili ya chai na chakula cha mchana.

Wakizungumza na waandishi wa habari nje ya viwanja vya chuo hicho juzi, walimu wanaoshiriki mafunzo hayo walisema wamegoma kuingia darasani kwa sababu viongozi wa mafunzo hayo wamewabadilishia utaratibu ambao ulizoeleka tangu awali.

Baada ya walimu hao kugoma kwa takribani siku nzima juzi, viongozi wanaosimamia mafunzo hayo wakiwamo maofisa kutoka TEA, walijaribu kuwasihi wakubaliane na malipo hayo ya posho ili kuendelea na mafunzo.

Kabla ya walimu hao kuanza mgomo, viongozi hao walikutana na wawakilishi wa walimu hao kwa lengo la kutafuta suluhu, lakini walimu walionekana kutoridhishwa na uamuzi uliochukuliwa na viongozi hao.

Mwakilishi wa walimu hao, Weni Msigwa, alisema kuwa katika kikao chao na waandaaji wa mafunzo, walikubaliana kila mshiriki alipwe posho ya Sh. 60,000 na kati yake, atakatwa Sh. 15,000 kwa ajili ya chakula chenye hadhi ya kiwango hicho cha fedha.

Hata hivyo, walimu hao hawakuridhia na kuanza kuzomea uamuzi huo huku wakisema "hatutaki chakula chao" licha ya Ofisa Taaluma Njombe, Steven kujaribu kuwasihi kurejea darasani.

Hadi Nipashe inaondoka eneo la tukio, majadiliano baina ya pande hizo mbili yalikuwa yanaendelea huku baadhi ya walimu wakitaka kulipwa fedha hizo haraka kwa madai kuwa wameshindwa kulipia vyumba kwenye nyumba za kulala wageni na wengine kudai kuwa tayari walikuwa wameweka rehani baadhi ya vifaa vyao zikiwamo simu za mkononi.

Mafunzo hayo ya elimu ya awali kwa mtaala mpya ni ya siku nane yakiwashirikisha walimu zaidi ya 900 kutoka mikoa hiyo miwili.

Habari Kubwa