Changamoto za uwekezaji kutatuliwa

28Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Shinyanga
Nipashe
Changamoto za uwekezaji kutatuliwa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki, amesema serikali itafanyia kazi changamoto na mapendekezo yote yaliyotolewa na wawekezaji mkoani Shinyanga. Pia ameahidi uboreshaji wa mazingira ya biashara na kuwekeza nchini.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki.

"Serikali itaendelea kuyaboresha mazingira ya biashara ikiwamo kupunguza kodi, tozo na ada mbalimbali ili kurahisisha  na kuvutia uwekezeji na biashara nchini," alisema Kairuki na kuongezea kuwa sheria mpya ya uwezeshaji itasaidia kulinda  na kuchochea ukuaji wa uwekezaji na biashara.

Akizungumza mjini Shinyanga katika mkutano wa wazi wa majadiliano kati ya serikali, wawekezaji na wafanyabiashara wa mkoa huo, aliwaondoa wasiwasi kuwa serikali  imeazimia kufikia uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025 sambamba na  kuweka  mazingira rafiki na wezeshi kwa uwekezaji na biashara kukua.

Kairuki alisema mikutano ya majadiliano moja ya mambo mengi inalenga kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji na wafanyabiashara ili kufanikisha azma ya serikali ya kujenga uchumi imara pamoja na kuvutia mitaji mikubwa katika biashara na  uwekezaji.

Aliwapongeza washiriki wa mkutano huo ambao waliibua hoja muhimu zilizopatiwa majawabu na manaibu  mawaziri katika sekta  husika, hivyo mapendekezo yote yaliyotolewa yatawasilishwa serikalini kupata ufumbuzi wa kudumu.

"Niziombe mamlaka za serikali ziwe na utaratibu wa kufanya ukaguzi kwa pamoja katika viwanda na maeneo ya biashara na uwekezaji ili kumwezesha afanye kazi zake kwa nafasi tofauti na hali ilivyo sasa kwani kila mamlaka huenda kwa wakati wake,” alisema Waziri Kairuki.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, aliwahakikishia wafanyabiashara kuwa kero zote zitafanyiwa kazi na kuzitaka taasisi za kifedha kujitafakari katika utoaji wa mikopo yenye riba kubwa wakati serikali ilishafanya maboresho katika riba.

"Serikali inawatoza wenye benki asilimia 7 ya riba ya mkopo kutoka benki, hivyo wanakila sababu ya kujitafakari juu ya riba wanazotoza kwa sasa ya zaidi ya asilimia 18 jambo ambalo siyo sahihi," alisema Dk. Kijaji.

Alisema zaidi ya kodi na tozo 164 zimefutwa na serikali ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, alisema mkoa wake umefanya jitihada kubwa ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ambapo hadi sasa kuna jumla ya viwanda 729 kati ya hivyo, 13 ni viwanda vikubwa, 11 viwanda vya kati na 705 ni viwanda vidogo ambavyo vimeajiri Watanzania 10,150.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, aliwahakikishia wafanyabiashara kuwa fursa ya uwekezaji katika sekta ya uvuvi na ufugaji ni kubwa katika Mkoa wa Shinyanga na kuwaomba kuwekeza zaidi katika sekta hiyo.

Habari Kubwa