Chanzo ajali ya Noah iliyoua 18 hapohapo

08Nov 2016
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Chanzo ajali ya Noah iliyoua 18 hapohapo

WATU 18 wamefariki dunia huku watatu wakijeruhiwa kwenye ajali ya gari dogo aina ya Noah lililogongana uso kwa uso na lori katika kijiji cha Nsalala kata ya Tinde, Shinyanga vijijini juzi usiku.

Ajali hiyo ilitokea saa 1:30 usiku wakati Noah hiyo yenye namba T 232 BQR ikitokea Nzega kwenda Tinde, ilipokuwa inalipita lori aina ya Fuso, kugongana uso kwa uso na lori lenye namba T 198 CDQ likitokea Kahama kwenda Dar es Salaam na kusababisha vifo hivyo papohapo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Jumanne Murilo alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Noah ambaye alikuwa akitaka kulipita Fuso ambalo lilikuwa mbele yake bila ya kuzingatia usalama na kusababisha watu hao 18 kupoteza maisha.

Aliwataja watu 10 waliotambuliwa kufariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Daudi Maja, Dina Masanja, Chausiku Kasapa, Specioza Doto na Ester Kasapa.

Wengine ni Vicent Nzamala, Emmanuel Jumanne, Maganga Lubala, Debora Maingu na Andrea Mambosasa.

Murilo alisema ndugu za marehemu walikuwa wakifanya maandalizi ya kwenda kuzika miili ya marehemu.

Alisema madereva wote, Seif Mohamed wa Noah na Aloyce Kavishe wa lori wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano juu ya kukiuka sheria za usalama barabarani na kupoteza maisha ya abiria hao na kusababisha majeruhi, na watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Daniel Maguja, alithibitisha kupokea miili ya marehemu 18 na majeruhi watatu ambao ni Hamisi Ally (5), Salima Kiiza (1) na Boniface Richard.

Alisema hali za majeruhi hao ni nzuri na wanaendelea kupatiwa tiba baada ya kuumia sehemu mbalimbali za viungo vya miili yao.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti jana, mashuhuda wa tukio hilo, Jamali Mohamed na Amos Tinde, walisema waliiona Noah hiyo ikitaka kulipita Fuso, lakini ikashindikana ndipo ikagongana na lori hilo likiwa katika mwendo kasi na kusabababisha vifo vya watu hao.

Mohamed alisema walishuhudia wanawake wanane, wanaume saba na watoto watatu wakiwa wamepata majeraha makubwa na baadhi yao walionekana walikuwa wameshapoteza maisha, lakini hawakuwa na uhakika kama wote walikuwa wamefariki.

Habari Kubwa