Chanzo vifo maofisa wa3 TIC

23May 2018
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Chanzo vifo maofisa wa3 TIC

MAOFISA waandamizi watatu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), wamekufa papo hapo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kwenda mkoani Dodoma kugongana uso kwa uso na lori katika kijiji cha Msata, Bagamoyo mkoani Pwani.

Ofisa Uhamasishaji na Uwekezaji wa TIC, Latifa Kigoda, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa ilitokea juzi saa 9:00 jioni.

Latifa aliwataja waliofariki ni Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti, Mipango na Tehama, Said Amiri, Kaimu Mkurugenzi wa Masuala ya Taasisi, Zacharia Kingu (49) na Meneja wa Utafiti, Martine Masalu (39).

Pia aliwataja majeruhi wa ajali hiyo ni Meneja wa Sheria, Godfrey Kilolo na dereva Priscus Peter (23) aliyekuwa akiendesha gari hilo lenye namba za usajili STK 5923 aina ya Toyota Land Cruiser GX 200.

Alisema watumishi hao walikuwa wakiwahi kuhudhuria kikao cha wataalamu wa Kamati ya Taifa ya Uwekezaji (NISC) ambacho kilikuwa kinafanyika jana asubuhi jijini Dodoma.

Akielezea namna ajali hiyo ilivyotokea, Latifa alisema dereva alikuwa akijaribu kukwepa shimo lililokuwa njiani walipofika kijijini Msoga na ndipo lilipokutana uso kwa uso na lori.

“Maiti zimehifadhiwa Hospitali ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi, Kibaha na utaratibu wa kuzihamishia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zinaendelea,” alisema.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Jonathan Shana, alilitaja lori lililogongana na gari hilo la serikali ni lenye namba za usajili T 620 AQV lenye tela T 407 DBY aina ya Scania ambalo dereva wake alikimbia baada ya ajali hiyo.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari la serikali kuhama kutoka upande wake na kwenda kugongana na lori hilo.

Alisema juhudi za kumsaka dereva wa lori hilo zinaendelea kufanyika na majeruhi wa ajali hiyo walipelekwa Hospitali ya Msoga na baadaye kuhamishiwa Muhimbili.

Taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ilieleza kusikitishwa na vifo hivyo na kufafanua kuwa taratibu za mazishi zinaendelea kufanyika.

Imeandikwa na Romana Mallya, Dar na Margaret Malisa, Kibaha.

Habari Kubwa