CHAUMMA yaahidi kujenga daraja Dar hadi Zanzibar

06Sep 2020
Thobias Mwanakatwe
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
CHAUMMA yaahidi kujenga daraja Dar hadi Zanzibar

MATUMAINI ya wananchi kupata ubwabwa na kuku wakati wa mikutano ya kampeni wa Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Hashimu Rungwe, yameyeyuka baada Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) kupiga marufuku utaratibu huo.

Vilevile, chama hicho kimeahidi kujenga daraja kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar ili wananchi waachane na usafiri wa meli na boti ambao kimesema siyo rafiki kwao.

Jana, katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho eneo la Manzese Bakhresa jijini Dar es Salaam jana, Rungwe hakutekeleza ahadi yake ya kutoa ubwabwa kwa wananchi kutokana na amri hiyo ya TAKUKURU aliyopewa juzi.

Taasisi hiyo nyeti ilionya kuwa kutoa chakula kwa wananchi kipindi hiki cha kampeni ni kosa kwa mujibu wa sheria. Rungwe alisema jana kuwa alipanga kutoa ubwabwa kwenye mkutano, lakini TAKUKURU wamempiga marufuku.

"Nilipanga chakula kije hapa kwenye mkutano, lakini TAKUKURU wamenikataza, hii roho mbaya tu," alisema Rungwe huku akionyesha kwa wananchi nakala ya Gazeti la Nipashe toleo la jana ambalo lilikuwa na habari ya TAKUKURU kumpiga marufuku mgombea huyo kugawa ubwabwa.

Rungwe alisema inashangaza TAKUKURU kuona suala la kutoa chakula ni rushwa wakati wakialikwa kwenye vikao mbalimbali vinavyoandaliwa na serikali ya CCM wanapewa chai, chakula na mshiko.

Alisema serikali yake itahakikisha inaongoza kwa utawala wa haki na kwamba wananchi watakaovunjia nyumba zao, watalipwa fidia tofauti na sasa ambapo hawalipwi.

"Sisi tunataka utawala wa haki, watu wafanye siasa za haki bila kuonewa," alisema na kuongeza kuwa serikali yake itatoa ajira kwa vijana kwa kuanzisha viwanda.

Mgombea mwenza, Mohamed Masoud Rashid, alisema sera za CHAUMMA ni bora kuliko chama kingine cha siasa nchini na mpango wao wa kupeleka bahari Dodoma wana imani utaporwa.

"Dodoma tangu itangazwe kuwa makao makuu ya nchi imechukua zaidi ya miaka 40 kuhamishia ofisi huko. Kwa hiyo, na sisi tumedhamiria kuipeleka bahari Dodoma ili kuunga juhudi hizo," alisema.

Rashid pia alisema wananchi wakikipa ridhaa chama hicho, serikali yake itajenga daraja kutoka Zanzibar hadi Dar es Salaam ili kurahisisha usafiri.

Habari Kubwa