CHAVITA, Simiyu yakiri kutowafikia walengwa

18Jun 2019
Happy Severine
Simiyu
Nipashe
CHAVITA, Simiyu yakiri kutowafikia walengwa

CHAMA cha Viziwi Mkoa wa Simiyu (CHAVITA) kimekiri kushindwa kuwafikia na kuwabaini walengwa wake kwa  asilimia 99 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa rasilimali fedha na rasilimali watu.

Mkarimani wa lugha ya alama Jonathan Livingstone akitoa ufafanuzi wa jambo kwa chama cha viziwi Mkoa wa Simiyu.

Akizungumza leo kwenye kikao cha majadiliano na Kamati za Ulinzi na Usalama za mkoani Simiyu, Mwenyekiti wa CHAVITA mkoani hapa Zephania Mhandi amesema  chama hicho kimeshindwa kuwafikia walengwa wao kwa sababu ya kutokuwa na rasilimali fedha za kutosha katika kuendesha shughuli zao.

Amesema kuwa lengo la majadiliano hayo ni kuweka usawa wa pamoja na kuhamasisha msukumo kwa sekta muhimu  ili kuwakomboa watu wenye ulemavu wa kusikia (viziwi).

Mhandi amesema kuwa  changamoto kubwa  inayolikabili kundi hilo ni kutokuwepo kwa  rasilimali fedha  na watu ambazo  zimefanya kushindwa kuwafikia walemavu wengine kwa asilimia 99 ambapo kwa sasa kutoa elimu ya lugha ya alama kwa kiwango kidogo chini ya ufadhili wa shirika la Foundation for Civil Society.

Ameongeza kuwa Chama hicho kimebaini  kuwa Taasisi muhimu za kiserikali ikiwemo Jeshi la Polisi, Magereza na Mahakama bado hazijatambua umuhimu wa kuwashirikisha Watu wenye Ulemavu katika shughuli za kijamii na Maendeleo ya taifa.

Nao baadhi ya wajumbe katika kikao hicho wamesema kanuni za watu wenye ulemavu (viziwi) zifikishwe kwenye taasisi na vyombo vya ulinzi na usalama ili ziweze kufahamika na pia mashirika ya uzalishaji na ukuzaji uchumi wapatiwe elimu ya utoaji misaada ili kuwajengewa uwezo na miradi ya kujiendesha kiuchumi.

Naye Katibu Tawala wilaya ya Meatu Godwin Chacha amesema elimu ya lugha za alama na kanuni za sheria ya haki na ulinzi zisiishie kutolewa kwa taasisi za kiserikali bali ziyafikie makundi yote katika jamii ikwemo mashirika ya kiuchumi.

Amesisitizakuwa fedha zilizoelekezwa na serikali kutenga na mashirika binafsi ili kuhudumia makundi maalumu zitolewe na zitumike kuwajengewa uwezo walemavu ili wajitokeze kuwania nafasi mbalimbali za kiuongozi kwenye chaguzi zijazo.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga aliwataka maofisa ustawi wa jamii kutoa mpango kazi utakaowezesha kila sekta kutekeleza mahitaji ya watu wenye ulamavu (viziwi).

Kiswaga amesema watu wenye ulemavu wana haki kama watu wengine hivyo ni lazima wapate haki sawa na wananchi wengine huku akiwasisitiza viziwi kutopita maeneo yenye ulinzi mkali na hatari.

Habari Kubwa