CHAVITA yaomba mtaala maalumu kufundisha wanafunzi viziwi

08Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
CHAVITA yaomba mtaala maalumu kufundisha wanafunzi viziwi

CHAMA cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), kimeiomba Idara ya Elimu nchini kuwa na mtaala maalumu wa kufundishia wanafunzi ambao ni viziwi mashuleni ili waweze kuendelea na elimu ya juu.

Hayo yamesemwa leo Juni 8, 2021 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Dickson Mveyange, wakati wa mafunzo na kampeni kuhusu ukiziwi na lugha ya alama yaliyohusisha wadau wa Elimu, wazazi wa watoto wenye ukiziwi na wadau wa maendeleo.

Mveyange amesema mitaala inayotumika mashuleni ni ya jumla na haiwazingatii viziwi pamoja na kuwa kuna tofauti ya wanaosikia na viziwi hali ambayo imekuwa ni kikwazo kwa watoto hao ambao wanatakiwa kupewa elimu maalum badala ya elimu ya jumla.

Amesema licha ya idara ya maendeleo ya jamii kuridhia kuwepo kwa lugha ya alama lakini inaonekana bado halijatekelezwa ipasavyo na kusababisha wanafunzi wengi viziwi kushindwa kuendelea na masomo Kutokana na ugumu wa lugha ya mawasiliano.

“Bado kuna mapungufu mengi, tunahitaji maboresho zaidi ili kuweka usawa kwa jamii na viziwi nao waweze kusoma bila kubaguliwa, bado ukosefu wa misamiati ya masomo ya sayansi, uraia na historia ni changamoto hivyo vinapaswa kuangaliwa upya,” amesisitiza Mveyange.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Taifa (CHAVITA), Nidrosy Mlawa, ameitaka jamii kuwashirikisha viziwi katika mambo yote ili maendeleo yasimwache mtu.

Habari Kubwa