Chenge afichua siri babu wa watoto 30

10Sep 2019
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
Chenge afichua siri babu wa watoto 30
  • *Asema ana wajukuu kibao, wawili ni wabunge, wenyewe wadai hawajuani...

ALIFARIKI dunia mwaka 1990 na kuacha watoto 30 na wajukuu zaidi ya 60. Ni Mzee Gulamali ambaye leo Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, amefichua kuwa ana wajukuu wawili ambao ni wabunge. 

Wakati wa kikao cha leo cha Bunge, Chenge amekiongoza, amelilipua Bunge kwa shangwe baada ya kueleza kuwa Mzee Gulamali alikuwa "mtu wa shughuli".

Chenge wakati akimtambulisha mmoja wa wake wa mzee huyo aliyekuwa ametembelea Bunge, amesema: "Naomba nimwelezee vizuri Mzee Gulamali, alifariki mwaka 1990, aliacha watoto 30 na wajukuu zaidi ya 60.

"Kwa hiyo, Mzee Gulamali alikuwa mtu wa shughuli... (kicheko kikatawala bungeni). Kati ya wajukuu hao, wawili tunao humu ndani ni wabunge, Seif Gulamali wa Manonga (CCM) na Hussein Amar, Mbunge wa Nyang'hwale (CCM)."

Nje ya Ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Manonga (Gulamali) ameweka wazi kuwa wajukuu wa Mzee Gulamali, yeye ikiwamo, ni wengi na hawajuani. 

"Kumbuka idadi ya wajukuu 60 iliyotumwa na Mheshimiwa Chenge ni ya mwaka 1990, na hao ni wale tuliokuwa nao kwenye msiba. 

"Tupo wengi sana na hatujuani. Kuna mwingine nimemjua mwaka huu, anatoka Tanga huko. Nilipomwona nilibaini mara moja kwamba huyu atakuwa ndugu yangu maana anafanana sana na mama yangu," amesema.

Habari Kubwa