CHF yaja na mpango mkakati kuinua vijana

13Sep 2021
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Nipashe
CHF yaja na mpango mkakati kuinua vijana

​​​​​​​TAASISI ya kiraia ya (Community hands CHF) imekuja na mipango mkakati ya kuwawezesha vijana katika nyanja mbalimbali ikiwa na dhumuni la kuwainua kiuelewa na kiuchumi ili wasiwe tegemezi katika jamii inayowazunguka.

Akizungumza na Nipashe mapema leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Paul Makoe, amesema, katika utafiti wao walibaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana katika jamii hali ya kushindwa kufikia malengo kwa kukosa maarifa au viwezeshi.

Amesema miongoni mwa vitu ambavyo wamevipa kipaumbele katika kuwasaidia vijana nchini ni katika nyanja ya kielimu, Afya, mazingira na kutetea haki za watoto, wanawake, na walemavu hususani viziwi.

“Taasisi hii iliona kuna uhitaji wa vijana kuwezeshwa kimaarifa, kutokana na matatizo yanayowakabili hususani suala la kukosa ajira hivyo tumekuja na miradi ambayo itaenda kujibu changamoto zao kwa kuwaongezea uelewa na kujua namna ya kujiajiri,” amesema Makoe.

Ameongeza kuwa kampuni hiyo inashirikiana na taasisi mbalimbali za vijana pamoja na vyuo vikuu, katika kuanzisha kituo cha ufundishaji mahususi kwa ajili ya kukuza mawazo ya vijana katika ubunifu wanaoufanya ili uweze kuwa na tija.

Aidha, taasisi hiyo pia imelenga kuwainua wanawake kwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali itakayowasaidia kujua ni namna gani ya kupangilia matumizi ya fedha katika kuendesha biashara ili waweze kufikia malengo.

“Katika utekelezaji wa hilo tumesha anza kuendesha makongamano ya vijana katika Mkoa wa Lindi na Morogoro vijijini, ikiwa ni moja ya kuiunga mkono serikali katika kuwawezesha vijana kujiajiri wenyewe na kupunguza tatizo la ajira nchini,” amesema Makoe.

Pia amesema tafiti zao zilifanikiwa kubaini uwepo wa uhaba wa vituo pamoja na vifaa vya kufundishia viziwi na tayari wamesha chukua hatua za awali katika kulitatua hilo kwa kutengeneza program inayopatikana katika vifaa vya kielektroniki itakayomuwezesha mtoto mwenye tatizo hilo kusoma, akiwa mahali popote.

Mbali na hilo ameeleza kuwa wameshirikiana na taasisi ya Wezesha Mafanikio, katika kutoa taulo za wanawake katika shule mbalimbali nchini ikiwa ni moja ya njia ya kuwasaidia kujisitiri wakati wa hedhi, huku wakiwasisitiza kuwa na utamaduni wa kulinda afya zao.

“Tunaiomba serikali pamoja na wadau na taasisi mbalimbali waweze kutuunga mkono katika miradi tuliyoianzisha na kuipendekeza ili kufikia malengo ya kuwawezesha vijana wengi zaidi nchini,” amesema Makoe.

Kongamano hilo la vijana lililofanyika leo mapema Posta jijini Dar es Salaam, liliandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo taasisi ya (Community Hands Foundation) ni miongoni mwa wadau waliohusika katika kujadili sera ya vijana inayotoa vipaumbele kwa kundi rika ikiwemo mafunzo ya ujasiriamali, elimu, uchumi, afya, mazingira na haki za binadamu. Jambo lingine walilojadili ni mipango mbalimbali ya kustawisha jamii na vijana kwa ujumla.