Chikota ataja mambo muhimu 5 Nanyamba

17Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Mtwara
Nipashe
Chikota ataja mambo muhimu 5 Nanyamba

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Nanyamba mkoani Mtwara kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Chikota, amezindua kampeni zake huku akitaja mambo muhimu matano atakayoyafanya endapo atachaguliwa.

Akizungumza jana kwenye uzinduzi wa kampeni za CCM, uliofanyika kwenye Kata ya Mtiniko, Chikota alitaja mambo hayo kuwa ni kuboresha sekta ya afya kwa kuongeza vituo vya afya, zahanati kwenye maeneo ambayo hayana na kukamilisha ujenzi wa majengo yaliyobaki kwenye ujenzi wa hospitali ya wilaya.

Kuhusu sekta ya maji, mgombea huyo alisema atahakikisha anasimamia ukamilishaji wa mradi wa maji ulioanza Nanyamba na Chawi.

“Nitahakikisha nafuatilia serikalini kuhusu uanzishaji wa mradi wa maji mkubwa, ili kusaidia kata tano ambazo zina shida kubwa ya maji zikiwamo Mnima, Nyundo, Timbwilimbwi, Njengwa na Nitekela,” alisema.

Akizungumzia sekta ya elimu, aliahidi kuendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu ya shule kwa kujenga madarasa, nyumba za walimu na matundu ya vyoo.

Kadhalika, alisema atahakikisha anasimamia serikali kukamilisha vijiji 52 ambavyo vimebaki bado havijapata umeme.

“Naomba mnichague tena kwa kipindi kingine cha miaka mitano, pia mchague Rais John Magufuli na wagombea wote wa CCM na madiwani wa kata zote 17 ili kuharakisha maendeleo ya Nanyamba.

“Katika miaka mitano iliyopita, mmeshuhudia mafanikio mengi kwenye sekta mbalimbali, miaka mitano ijayo pia nitasimamia serikali kuongeza fedha zinazotengwa kwa ajili ya TARURA kukamilisha miradi ya barabara vijijini na kuweka lami kwenye vilima korofi,” alisema.

Katika mkutano huo, mgombea huyo alitaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kuwa ni ujenzi wa hospitali ya wilaya iliyogharimu zaidi ya Sh. bilioni moja, ujenzi wa vituo vya afya vitatu vya Majengo, Dinyecha na Kilomba vilivyogharimu Sh. bilioni 1.4.

“Kuna ujenzi wa zahanati 11 unaendelea, lakini halmashauri imepata magari matatu ikiwamo gari moja la mganga mkuu na mengine ya wagojwa (ambulance),” alisema.

Pia alisema wananchi wamenufaika na ujenzi wa barabara ya Mtwara-Mnivata kwa kiwango cha lami unaoendelea na barabara za mzunguko za ndani katika halmashauri ambapo kila mwaka zinajengwa kilometa mbili kwa kiwango cha lami hivyo kufikia kilometa 11 .8 huku Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) likijenga minara 11 ya simu.

“Kwa hiyo ndugu zangu mnaona dhahiri mafanikio na faida inayofanywa na CCM tusifanye makosa mara mbili, tufanye maamuzi sahihi tuchague Chama Cha Mapinduzi ili tuzidi kunufaika na maendeleo katika halmashauri yetu na mkoa kwa ujumla," alisema Chikota.

Habari Kubwa