China yaipa Tanzania msaada bil. 60/-

25Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
China yaipa Tanzania msaada bil. 60/-

TANZANIA imetia saini mkataba wa kupatiwa fedha za msaada wa Sh. bilioni 60 za Kitanzania kutoka Serikali ya Watu wa China bila ya masharti yoyote.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, akibadilishana nyaraka na Makamu Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la China, Zhou Liujun, baada ya kusaini mkataba wa msaada wa Sh. bilioni 60, zilizotolewa na nchi hiyo kwa Tanzania, bila ya masharti yoyote, katika hafla iliyofanyika, mjini Beijing, China jana. PICHA: WIZARA YA MAMBO YA NJE

Katika mkataba huo, taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa vyombo vya habari ilisema kupitia fedha hizo,  Serikali ya Tanzania itaamua matumizi yake katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wake. 

Mkataba huo ulitiwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, kwa niaba ya Tanzania na Makamu Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la China,  Zhou Liujun kwa upande wa Serikali ya China.

Taarifa hiyo ilisema mkataba huo ulitiwa saini baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya Prof. Kabudi na Waziri wa Mambo ya Nje wa China na Mjumbe wa Baraza la Taifa, Wang Yi.

Mazungumzo ya mawaziri hao yalilenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya China na Tanzania sambamba na kuibua maeneo ya kipaumbele na kimkakati yatakayotekelezwa kwa ushirikiano baina ya pande hizo.

Maeneo hayo, kwa mujibu wa taarifa hiyo  ni pamoja na upembuzi yakinifu kwa ajili ya upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ili kuwa  Taasisi Mahiri ya Tiba ya Moyo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Maeneo mengine ya kimkakati ni ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha umeme ya Ruhudji (megawati 358) na Rumakali (megawati 222) yaliyoko Iringa na Njombe ambayo yote kwa pamoja yatakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa takribani megawati 580,  upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa na ukarabati wa reli ya Tazara.

Aidha, katika mazungumzo yao, serikali ya China imeahidi pia kuunga mkono katika ujenzi wa miundombinu muhimu katika mji mpya wa serikali katika makao makuu Dodoma.

Taarifa hiyo pia ilisema Waziri Wang alisifu uhusiano mwema na wa kirafiki baina ya Tanzania na China na kuongeza kuwa Tanzania imekuwa rafiki wa kweli wa China kwa wakati wote.

Prof. Kabudi kwa upande wake, aliishukuru serikali ya China sambamba na kueleza kuwa kipaumbele cha Tanzania ni kudumisha na kuendeleza uhusiano mzuri wa kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi uliopo baina ya nchi hizo mbili kwa manufaa ya pande zote mbili.

Pia Prof. Kabudi aliipongeza serikali ya China na nchi za Afrika kwa kuandaa mpango kazi wa kimkakati ambao umeainisha maeneo 10 ya kipaumbele yakiwamo uendelezaji wa sekta ya viwanda na miundombinu ambayo kwa Afrika hususan Tanzania ndicho kipaumbele cha kwanza.

Maeneo mengine ya kipaumbele ni pamoja na uendelezaji wa biashara na uwekezaji kati ya China na Afrika pamoja na ushirikiano katika maeneo ya ulinzi na usalama.

Habari Kubwa